Wahariri Tanzania wampongeza Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa SADC

0
28
By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limempongeza Rais John Magufuli wa Tanzania kwa kuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Nafasi hiyo ya uenyekiti unarejea Tanzania baada ya miaka 16, ikiwa ni mara ya pili tangu mwaka 2003.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Agosti 15, 2019 na Kaimu Mwenyekiti TEF, Deodatus Balile inaeleza nafasi hiyo ni heshima kwa taifa ambapo Rais Magufuli atapata fursa ya kuongoza nchi 16 ambazo zina watu zaidi ya milioni 350.

“TEF tunaona fahari kwa Taifa letu kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa 39 wa wakuu wa nchi za SADC, tunaungana na wapenda amani na maendeleo wote kuutakia kila la kheri mkutano huu utakaofanyika Agosti 17 na 18, 2019 jijini Dar es Salaam ukiwa unabeba kaulimbiu isemayo ‘Mazingira Wezeshi kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda,” amesema Balile

Taarifa hiyo inaeleza kuwa SADC ni taasisi yenye mizizi mirefu na hasa chimbuko lake ambalo ni hapa Tanzania kutokana na mkutano wa Julai, 1977 jijini Arusha.

Lengo mahususi la kuanzishwa SADC katika hatua mbalimbali lilikuwa ni ukombozi ambapo zilianza harakati za kupigania uhuru kwa nchi za Kusini mwa Afrika na baada ya kazi hii kukamilika SADC imeendeleza mapambano ya kupata ukombozi wa kiuchumi.

Ipo miungano kadhaa iliyoundwa awali, ikiwamo Kamati ya Ukombozi na Umoja wa Nchi za Mstari wa Mbele zilizopinga ubaguzi wa rangi kwa nchi za Afrika Kusini na Rhodesia (Zimbabwe).

Taarifa hiyo inasema Tanzania ikiwa nchi kiongozi, chini ya uongozi shupavu wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliwapa hifadhi wapigania uhuru wa Chama cha African National Congress (ANC) na Pan African Congress (PAC) vya Afrika Kusini, Mozambique Liberation Front (FRELIMO), People’s Movement for the Liberation of Angola (MPLA), Zimbabwean African National Union (ZANU), Zimbabwean African People’s Union (ZAPU), na South West Africa People’s Organisation (SWAPO) kutoka Namibia.

Jukwaa hilo limewakaribisha wakuu wa nchi za SADC katika mkutano wa 39 nchini Tanzania na kuwaomba watumie fursa hii kujiridhisha iwapo nchi zetu zimefikia malengo haya ya kupigania uhuru.

“Tunarejea kumpongeza Rais Magufuli kwa kushika wadhifa huu muhimu wa Uenyekiti wa SADC na tunaamini kwa dhana hii ya viwanda kwa nchi za SADC mataifa yetu yataelekea katika ukombozi wa kweli wa kiuchumi, ambao unapaswa kwenda sambamba na haki nyingine katika nchi zetu kama zilivyoainishwa katika Tamko la Haki za Binadamu la Mwaka 1948,”amesema.

Source: mwananchi