Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, CUF yatoa masharti kushirikiana na vyama vingine

0
41
By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama upinzani nchini Tanzania cha (CUF) kimesema kipo tayari kuungana na chama kingine cha upinzani katika kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi wa serikali za mitaa lazima wote wawe na lengo moja.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi ya Septemba 7, 2019 katika mkutano na waandishi wa habari uliokuwa umelenga kutoa msimamo wao kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Bunge na Sera, Mohammed Ngulanagwa amesema watakuwa tayari kushirikiana na chama chochote ambacho kitakwenda kwa dhati na dhamira yake inaonyesha ni kuwa tayari kuing’oa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani.

“Sisi tutakuwa na muungano na mtu yoyote ambaye hata kwa ndani dhamira yake ni kuing’oa CCM madarakani na siyo kusimama jukwaani kuongea kitu kingine huku akipita katika maeneo ambayo yanaongozwa na upinzani kupiga kampeni CCM ipite,” amesema Ngulangwa

Amesema muunganiko wa baadhi ya vyama vya upinzani uliokuwepo mwaka 2015 ulikuwa na upungufu mwingi ambapo yalitokana na wote kutokuwa na lengo moja katika vinywa na malengo yao

“Watu wenye malengo tofauti wakiungana wataishia kuparaganyika tu, wapinzani wa kweli wenye uwezo wa kuungana ni wale watakaosaidia kuhakikisha maeneo yao hayapotei.”

Advertisement

“Leo utakapoona mpinzani mmoja anaenda kujiimarisha kwenye himaya ya upinzani huyo lengo lake itakuwa ni kuisaidia CCM kupita,” amesema Ngulangwa

Vyama  ambavyo Ngulangwa anavizungumzia zilivyoungana mwaka 2015 ni NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF  vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Source: mwananchi