OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Wayahudi waanza kuishambulia Entebbe-8

0
51

Mara tu baada ya ndege ya kwanza ya kijeshi kutua, mkuu wa operesheni ya kuivamia Entebbe, Brigedia Jenerali Dan Shomron, aliwatawanya wapiganaji wake. Gari aina ya Mercedes Benz wailiyotoka nayo Israel ikiwa na rangi kama za ile ya Rais Idi Amin huku ikiwa na bendera ya Uganda, ilishushwa kwenye ndege na kuendeshwa kwa kasi kupita maeneo yaliyokuwa yanalindwa na wanajeshi wa Uganda katika uwanja wa Entebbe. Milango ya gari hilo ilipofunguliwa baadhi ya wanajeshi wa Uganda walipiga saluti wakidhani kuwa hilo ni gari la Rais wa Uganda.

Wakati wakiamini hivyo, makomandoo wa Israel waliokuwa kwenye gari hilo walishuka kwa ghafla wakiwa na bastola. Kufumba na kufumbua walinzi wote waliokuwa kwenye mnara wa zamani wa kuongozea ndege wakawa wameuawa. Ujanja wa kutumia gari linalofanana na la Idi Amin ukawa umefaulu katika hatua ya kwanza na muhimu.

Wakati hilo likitokea, ndege ya pili ya Israel ndiyo kwanza ilikuwa inatua uwanjani ikiwa na mkuu wa kikosi cha kuwaokoa mateka, Yonathani Netanyahu, pamoja na wapiganaji wake. Tayari walikuwa wamejipaka rangi nyeusi kuwapumbaza Waganda wasiwagundue kwa haraka.

Hata hivyo, wakati ndege ya pili inatua, inaelekea askari mmoja wa Uganda aliyekuwa kwenye mnara wa kuongozea ndege aliiona na kuitilia shaka. Ghafla taa zote za uwanja wa ndege wa Entebbe zikazimwa.

Lakini kuzimwa kwa taa hizo kulimsaidia zaidi rubani wa ndege ya nne na ya mwisho kutua uwanjani hapo. Kwa kuwa sasa risasi zilikuwa zimeshaanza kurushwa na askari wa Uganda walikuwa na hofu, ilikuwa ni rahisi zaidi kwa rubani wa ndege ya mwisho kutua katika giza kuliko angetua wakati taa za uwanja huo zikiwaka.

Baada ya rubani wa ndege ya mwisho kutua alikaririwa akisema: “Kutua gizani ndicho tulichofundishwa. Kwangu ilikuwa salama zaidi kutua katika giza totoro. Kwa kweli nilikuwa nimeanza kuingiwa na hofu baada ya kuona taa za uwanja zinawaka, lakini nilifarijika nilipoona zimezimika ghafla. Kazi yangu ilikuwa ni kutulia hadi wapiganaji wote waondoke ndani ya ndege halafu nianze kazi ya kuteketeza ndege za kijeshi zilizotengenezwa Urusi. Nilikaa ndani ya ndege kwa dakika 90, na hizo zilikuwa ni dakika ndefu kuliko zote nilizowahi kuishi kwa sababu wakati natua tu uwanjani mapambano yalianza na kudumu kwa dakika 90.”

Advertisement

Mjini Tel Aviv, waziri mkuu na baraza lake la mawaziri walikuwa ofisini kwa Shimon Peres ambako kulikuwa kumefungwa vifaa vya kusikiliza mapambano yaliyokuwa yanaendelea Entebbe. Ilipotimu saa 5:03 usiku wakasikia milio ya risasi ndipo wakajua kazi imeanza.

Wakiwa umbali wa zaidi ya maili 2,500 maofisa hao waandamizi wa Israel walikuwa wakisikiliza mapambano yalivyokuwa yakiendelea katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

Brigedia Jenerali Shomron alifanikiwa kusogea hadi lilipokuwa jengo wanamokaa abiria. Kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu wa operesheni hiyo, sasa kila kitu kilikuwa mikononi mwake. Komandoo mmoja wa Israel alifanikiwa kupenya na kukaribia jengo walimokuwa wanashikiliwa mateka. Msichana wa Kijerumani ambaye kwa wakati huu alikuwa ni mmoja wa magaidi waliokuwa wakiwalinda mateka aliitwa Gabriele Kroche-Tiedemann. Mwenzake, ambaye ni mwanaume na Mjerumani pia, aliitwa Wilfried Bose. Komandoo wa Israel alimwona Wilfried akiwa amesimama nje ya dirisha mojawapo la jengo hilo na hakujua hatari iliyokuwa inamjia. Wilfried alikuwa amebeba bunduki na bomu la kutupwa kwa mkono.

Ndani ya jengo hilo Myahudi mmoja mateka, Baruch Gross, aliyekuwa na umri wa miaka 41 alikuwa na mkewe aliyeitwa Ruth huku wakiwa wamembeba mtoto wao mwenye umri wa miaka sita aliyeitwa Shai, walikuwa macho.

Inaelezwa kuwa Gross mwenyewe hakupata usingizi tangu Idi Amin alipotangaza kuwa walikuwa wakisubiri kauli ya mwisho kutoka serikali ya Israel kabla ya saa sita usiku. Ilielezwa kuwa kama Israel haingetekeleza matakwa ya watekaji nyara, basi kuanzia siku inayofuata Jumapili, mateka wangeanza kuuawa mmoja baada ya mwingine. Hilo lilimfanya Gross asipate usiingizi. Huku akimtazama gaidi wa Kijerumani aliyekuwa amesimama nje dirishani akiwa amewaelekezea mateka bunduki yake aina ya Kalachnikov, Gross aliamini kuwa wakati wowote gaidi huyo angeanza kuwafyatulia risasi. Lakini wakati Gross akimtazama Mjerumani huyo, ghafla akaona bunduki aliyoshika ikidondoka na yeye mwenyewe kuanguka huku damu zikimwagika. Mara akasikia milio ya risasi ikirindima.

Wakati Gross akiendelea kushangaa, akaona mtu mmoja akiuruka mwili wa gaidi wa Kijerumani huku akikimbia kwa kasi. Gross hakuwa ametambua kuwa Waisraeli wameingia Entebbe. Akamkumbatia mtoto wake na kisha akamwambia mke wake wajifiche.

Komandoo wa Israel akasimama kwa sekunde chache akihema kwa nguvu. Akiwa amejibanza na ukuta, alimwona msichana wa Kijerumani, Gabriele, akirandaranda mbele ya mateka. Alikuwa ameshika bunduki kwa mkono mmoja na bomu la kutupwa kwa mkono likiwa limeshikwa na mkono mwingine.

Komandoo huyo wa Israel aliyetajwa kwa jina moja tu la Ilan, alinyanyua bunduki yake aina ya submachine gun na kummiminia risasi nyingi mwanamke huyo. Ilan alikuja kukiri baadaye kuwa katika maisha yake yote ya mapigano hakuwahi kumuua mwanamke, hasa kwa kumpiga risasi. Akiwa katika hali ya hofu, Ilan aliuruka mwili wa mwanamke huyo na kuingia chumba cha kupumzikia abiria.

Wakati wapambanaji wa kikosi cha Yonathan Netanyahu wakiingia chumba hicho, makomandoo waliokuwa kwenye ndege ya tatu ya Israel tayari walikuwa wameshalifikia jengo hilo. Amri zote zilitolewa kwa lugha ya Kiyahudi: “Laleni chini! Laleni chini haraka … Chini haraka.” Mateka walijikuta katika hali ya kuchanganyikiwa. Hata hivyo, pamoja na kwamba walikuwa katika hali ya taharuki, walielewa maana ya amri hiyo wakalala chini haraka.

Wapelestina wawili—Fayez Abdul-Rahim Jaber na Abed el Latif—walikuwa na mateka hao na wakasikia amri hiyo iliyotolewa kwa Kiyahudi. Walikuwa na bunduki tayari na wakaanza kufyatua risasi. Hata hivyo, makomandoo wa Israel waliwaona na kuwamiminia mvua ya risasi. Kilichowafanya wagunduliwe ni kitendo chao cha kunyanyua tu bunduki zao na kuanza kufyatua risasi ambazo ziliwajeruhi baadhi ya mateka. Lengo lao ni kuwalenga makomandoo wa Israel, lakini wakasambaratishwa.

Mmoja wa mateka, Ida Borochovitch, aliyekuwa na umri wa miaka 56, alivuja damu nyingi kutokana na kupatwa na risasi zilizorushwa. Mtoto wake, Boris Shlein, alisema alimwona gaidi mmoja akimfyatulia mama yake risasi sekunde chache kabla hajauawa.

Lizette Hadad, mateka mwingine, baadaye alisema: “Ghafla nikaanza kuona vitu kama makombora yakianguka kupitia darini. Yalinijeruhi. Muda mfupi baadaye Ida Borochovitch akaniangukia—na hiyo ndiyo ilikuwa salama yangu.”

Yosef Hadad, ambaye ni mume wa Ida, akasema: “Tulikuwa tumelala kama kawaida yetu. Tulikuwa tumelalia magodoro yaliyotandazwa sakafuni. Tulijaribu kulala lakini hatukupata usingizi. Wanajeshi walipoingia nilichukua kiti na kujikinga nacho kichwani. Nilihisi tu yule msichana wa Kijerumani alikuwa amejiandaa kutuua kwa sababu alikuwa ameelekeza bunduki yake kwetu, na aliposikia milio ya risasi alitaharuki. Nilifikiri maisha yetu yamefikia mwisho. Lakini ghafla nikamwona yule mwanamke wa Kijerumani ameanguka chini huku akivuja damu nyingi mwilini…”

Mateka mwingine, Benny Davidson alisimulia hivi: “Sikujua kama wavamizi walikuwa ni wanajeshi wa Israel. Ghafla tulisikia milio ya risasi. Tulikimbilia chooni. Kila mmoja alikuwa anakimbilia huko. Tuliposikia amri kwa lugha ya Kiyahudi tulichimbia vichwa vyetu sakafuni. Baba yangu alimlalia kaka yangu kumkinga, na mama yangu alinikinga mimi.”

Itaendelea kesho

Source: mwananchi