OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Mkuu wa kikosi cha uokoaji cha Israel auawa Entebbe-9

0
25

Chumba chote cha abiria katika uwanja wa zamani wa Entebbe kilijaa moshi uliotokana na risasi zilizofyatuliwa. Baadhi ya mateka waliingia chini ya magodoro wakati makomandoo zaidi walipokuwa wanazidi kuongezeka katika chumba hicho wakipiga kelele “Israel! Israel! Israel! Israel!”na kisha, wakitumia lugha ya Kiyahudi, wakawaamrisha mateka waendelee kulala chini. Ingawa wengi walilala, watoto wadogo hawakujua la kufanya. Wengine waliendelea kusimama na ndipo baadhi ya wazazi wao walipowarukia na kulala nao.

Mojawapo ya mablanketi lilipata moto kutokana na risasi za moto zilizokuwa zikirushwa. Arye Brolsky ni mmoja wa mateka aliyewakinga binti zake wawili kwa kuwalalia. Lakini mmojawao alikuwa karibu na blanketi lililoshika moto. Binti huyo aliponyanyuka tu kuukwepa moto huo akajeruhiwa kwa risasi.

Mashambulizi ya risasi katika chumba hicho yalidumu kwa jumla ya dakika moja na sekunde 45. Katika chumba hicho aliyeuawa ni kijana mmoja wa miaka 19 aliyeitwa Jean-Jacques Maimoni. Alipigwa risasi katika zile sekunde za mwanzo kabisa za mashambulizi ya risasi.

Kiongozi wa kikosi cha uokoaji, Yonathan Netanyahu na watu wake wakaanza kupekua kila mahali kuhakikisha wanawateketeza magaidi wote. Waligundua kulikuwa na magaidi wawili wenye silaha wakiwa wamejificha katika mojawapo ya vyoo vya jengo hilo. Kikosi kingine cha makomandoo, wakiwa katika mapambano upande mwingine wa jengo hilo walimkuta gaidi wa saba—Jayel Naji al-Arjam. Wote hawa waliuawa.

Madaktari wa Israel—watano wakiwa ni raia na wanne wakiwa ni wa Jeshi la Israel (IDF)—waliingia katika jengo hilo kuwabeba majeruhi na kuwapeleka kwenye ndege ya pili iliyokuwa na vifaa vya tiba.

Mapambano katika uwanja huo yakaingia hatua ya pili. Waisrael walianza kushambuliwa kutoka upande mmoja wa uwanja huo, lakini kikosi cha Yonathan Netanyahu kilijitahidi kukabiliana na washambuliaji.

Advertisement

Wakati mapambano yakiendelea, ikasikika sauti: “Yonni (Yonathan) amejeruhiwa! Yonni amepigwa risasi!” Yonathan alipigwa risasi ya mgongoni na kuanguka kifudifudi huku akibubujikwa na damu nyingi. Alipigwa risasi akiwa kwenye langu kuu la uwanja huo.

Alijaribu kusimama lakini alianguka tena. Akajaribu kusimama kwa mara ya pili lakini safari hii alianguka chali na kupoteza fahamu. Aliyekuwa akimfuatia kwa cheo aliripoti tukio hilo kwa Kamanda mkuu wa operesheni hiyo, Brigedia Jenerali Dan Shomron. Lakini huo haukuwa mwisho wa mapambano.

Kulikuwa na operesheni kadhaa zilizokuwa zinaendelea uwanjani hapo. Kila ndege ya Israel ilikuwa inalindwa na makomandoo 12 au zaidi. Kufikia hatua hii ndege ya pili ilikuwa imeshageuzwa tayari kuwabeba mateka na kuondoka. Ndege za jeshi la Uganda zilizokuwa uwanjani hapo zilianza kuteketezwa kwa kulipuliwa na makombora ya Israel yaliyorushwa kutoka kwenye magari ya kijeshi ya Israel ambayo yalikuwa yamebebwa na mojawapo ya ndege zao.

Waisrael walitarajia kukabiliana na upinzani mkali kutoka kwa majeshi ya Idi Amin ambayo waliamini hadi muda huo yalikuwa njiani yakitokea Kampala.

Kwa muda mfupi wa sekunde chache tu Waisrael walifika lango kubwa la uwanja mkubwa wa Entebbe na kushambulia. Shambulio hilo lilianza saa 6:01 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Mmoja wa waliosikia milio ya risasi na mabomu ni mwanadiplomasia wa Uingereza nchini Uganda, James Horrocks. Akiwa balozi mdogo wa Uingereza nchini humo alikuwa akifuatilia kwa karibu sana kutekwa kwa Ndege 139 ya Ufaransa ambayo sasa ilikuwa Entebbe, Uganda. Pia alikuwa akifuatilia sana habari za afya ya Dora Bloch, mwenye umri wa miaka 75, ambaye ni mmoja wa mateka lakini kwa sasa alikuwa amelazwa Hospitali ya Mulago mjini Kampala kwa matibabu. Dora alikuwa ametekwa pamoja na mtoto wake, Han Hartuv.

Alipelekwa hospitali Ijumaa, siku moja kabla makomandoo wa Israel hawajaivamia Entebbe. Mtoto wake alitarajia mama yake angerudishwa ili aungane na mateka wenzake. Dora na mwanawe walikuwa safarini kwenda New York, Marekani kuhudhuria harusi ya mtoto wake mwingine, Daniel, ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Wayahudi huko Marekani.

Usiku wa manane wa Jumamosi kuamkia Jumapili, James Horrocks alisikia sauti kubwa ya milipuko katika uwanja wa ndege wa Entebbe. Hakuwa na habari zozote kuhusu operesheni hiyo, hata za kijasusi kutoka Uingereza, jambo linaloeleza kuwa operesheni hiyo iliandaliwa kwa usiri mkubwa sana hadi ilipokuja kutekelezwa.

Kwa mujibu wa kitabu ‘Creative Thinking in Warfare’ cha Brigadier J Nazareth, uharibifu wa ndege za kijeshi zilizotengenezwa Urusi aina ya ‘Migs’ ulifanywa na timu ya wataalamu. Timu nyingine ya uharibifu ilikimbilia ilipokuwa radar kubwa uwanjani hapo. Walichofanya waliondoa vifaa muhimu katika radar hiyo iliyotengenezwa Urusi na kisha kulipua kituo kizima kupoteza ushahidi kuwa kuna vifaa viliondolewa.

Hadi kufikia hatua hii, miongoni mwa magaidi 10, saba walikuwa tayari wameuawa katika operesheni. Makomandoo wa Israel walichukua picha na alama za vidole za magaidi hao. Waandishi wawili wa historia—William Stevenson na Uri Dan—katika kitabu chao walichokiita ‘90 Minutes at Entebbe’ waliandika hivi: “Inaonekana magaidi wengine watatu, licha ya kwamba Waisraeli walikana, walichukuliwa hai kwa ajili ya mahojiano” nchini Israel.

Waisraeli walitaka kujaza ndege zao mafuta katika uwanja wa Entebbe lakini wazo hilo likaachwa kwa sababu walitaka kuondoka katika ardhi ya Uganda haraka iwezekanavyo. Ndege iliyowabeba mateka iliondoka uwanjani hapo ndani ya dakika 53 tangu ilipotua. Awali ilikuwa imepangwa ingeondoka ndani ya dakika 55. Kwa hiyo Waisrael walikuwa wamevuka matarajio yao kwa kutimiza lengo lao dakika mbili kabla ya muda uliokuwa umepangwa.

Mashambulizi makali ya silaha za kivita yalitawala uwanja wa Entebbe. Hatari kubwa zaidi ilikuwa ni milipuko iliyotokana na zile ndege za kijeshi za Uganda zilizokuwa zinalipuliwa na Waisrael. Katika hali hiyo, mkuu wa operesheni ya kuivamia Entebbe, Brigedia Jenerali Dan Shomron, alilazimika kufanya uamuzi wa haraka haraka. Ndege moja ambayo ilikuwa na mafuta ya kutosha kusafiri kwa dakika 90 tu ilikuwa lazima isafiri moja kwa moja hadi Nairobi. Ndege hiyo ingesafiri kwa dakika 50 kutoka Entebbe hadi Nairobi.

Zana zote zilizotumika katika operesheni hiyo ambazo walikuja nazo yakiwamo magari waliyokuja nayo, ushahidi wowote kuhusu washambuliaji (isipokuwa karakana zilizotumiwa, pampu kubwa ya mafuta ya ndege, na uharibifu wa jumla) viliondolewa na kikundi cha mwisho kuondoka uwanjani hapo.

Rubani mwandamizi wa ndege za Israel katika operesheni hiyo alikuwa amekaa ndani ya ndege yake kwa zaidi ya dakika 80 wakati wote mapambano makali yakiendelea, akijua wazi kombora lolote dhidi ya ndege hizo lingeweza kuvuruga operesheni yote.

Baadaye alikaririwa na mwandishi Uri Dan akisema “Nilijihisi upweke sana, na kila dakika ilionekana kama ni ya milele … Ilionekana kama muujiza kwamba ndege zetu hazikukutwa na matukio ya kushambuliwa. Tulipanga ratiba nzuri na ilikwenda vizuri sana. Akili yangu iliniambia kuwa kila kitu kilikuwa kikienda kwa kadiri kilivyopangwa lakini tumbo langu likaniambia kila kitu hakiwezi kuwa kamili—na wewe ndiye wa mwisho uliyebakia.”

Itaendelea kesho…

SOMA ZAIDI

Source: mwananchi