OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Idi Amin ajikakamua, aomba tena msaada Israel-11

0
22

Katika mazungumzo ya simu kati ya Idi Amin mjini Entebbe, Uganda na Baruch Bar-Lev mjini Tel Aviv, Israel, Bar-Lev aliripoti baadaye kuwa sauti ya Idi Amin ilikuwa ya taharuki. Hata hivyo Amin hakuwa amejua kwahakika kilichotokea Entebbe.

Awali Idi Amin alimlalamikia sana Bar-Lev akimuuliza, “Mmenitenda nini? Kwanini mmewaua askari wangu? Niliwatunza Waisraeli, niliwatendea vizuri, nikawapa huduma, blanketi, magodoro, nilitarajia kwamba hivi karibuni tutawaachia kwa kubadilishana lakini tazama mmewaua askari wangu.”

Amin: Wamewaua watu wangu.

Bar-Lev: Nani kawaua? Kwani mateka walikuwa na bunduki?

Amin: Si mateka wamewaua. Kuna ndege zimekuja na kuwaua.

Bar-Lev: Ndege? Sijasikia kama kulikuwa na ndege. Umeniamsha usingizini. Niko nyumbani na sijui chochote.

Advertisement

Hatimaye Idi Aman alianza kujikakamua wakati akizungumza na Bar-Lev. Inaonekana kuwa nia ya Bar-Lev ilikuwa ni kuumiza zaidi hisia za Idi Amin.

Baada ya mazungumzo marefu kiasi, Bar-Lev akamuuliza Idi Amin kama anaweza kuzungumza na mkewe, yaani mke wa Baruch Bar-Lev aliyeitwa Nehama ambaye alifahamiana sana na Amin. Hata hivyo Idi Amin alikataa kuongea na mke wa Bar-Lev na badala yake akamwambia amsalimie yeye na watoto wake. Bar-Lev akamwambia atamfikishia salamu zake.

Kwa waliosoma habari za mazungumzo kati ya Idi Amin na Bar-Lev na wakasikia Bar-Lev akimwambia Amin kama angependa kumsalimia mkewe ataamini kuwa Bar-Lev alikuwa nyumbani kwake na familia yake wakati wa mazungumzo hayo. Inaelekea hata Idi Amin aliamini hivyo pia.

Lakini mwandishi Louis Williams, katika ukurasa wa 129 wa kitabu chake, ‘The Israel Defense Forces: A People’s Army’, ameandika hivi: “Mkutano huo ulifanyika ofisini kwa (Waziri wa Ulinzi, Shimon) Peres ambako alikuwa na wanajeshi wachache sana wa Jeshi la Israel (IDF) waliofahamiana sana na Idi Amin.

“Taratibu lakini kwa uhakika, Peres alikuwa akicheza na saikolojia ya dikteta wa Afrika… kama ilivyokuwa imepangwa, kanali mstaafu wa IDF, Burka Bar-Lev, alipelekwa chumba kingine wakati simu ikipigwa Uganda (kwa Amin) … Bar-Lev alielekezwa acheze na nafsi ya Amin ili kwa kujuana kwao zipatikane habari zaidi kuhusu anachokijua na anachokitaka … Wakati wa mazungumzo yote Peres alikuwa akisikiliza kwa makini huku akiandika kila kitu muhimu kilichosemwa na Amin.”

Katika ukurasa wa 61 wa kitabu chake, ‘Operation Thunder, The Entebbe Raid: The Israelis Own Story’, mwandishi wake, Yehuda Ofer, anasema Bar-Lev na Nehama—pamoja na watoto wao wanne—walikuwa marafiki sana wa familia ya Idi Amin tangu mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970. Kufahamiana huko kulitokana na Bar-Lev kukaa Uganda kama mwambata wa kijeshi wa Jeshi la Israel (IDF).

Ushuhuda huo unatolewa pia na mwandishi Dani Wadada Nabudere katika ukurasa wa 312 wa kitabu chake alichokiita ‘Imperialism and Revolution in Uganda’. Miaka mitatu baadaye huyu Nabudere alikuja kuwa Waziri wa Sheria wa Uganda baada ya Idi Amin kuondolewa madarakani na majeshi ya Tanzania.

Hata kitendo cha Milton Obote kupinduliwa na Idi Amin Jumatatu ya Januari 25, 1971 kilitokana na kusaidiwa sana na Shirika la Kijasusi la Israel (Mossad), ambalo kiongozi wake nchini Uganda alikuwa ni Baruch Bar-Lev.

Kwa mujibu wa mwandishi Benjamin Beit-Hallahmi katika ukurasa wa 62 wa kitabu chake, ‘The Israeli Connection: Who Israel Arms and Why,’ Waisraeli walikuwa wameanza kutishwa na mabadiliko ya tabia ya kisiasa ya Obote ya kuupinga Uyahudi. Beit-Hallahmi anaandika: “ (Idi) Amin, (Waisraeli) waliwaza, angekuwa kibaraka wao mzuri sana na angeishi maisha yake ya kisiasa kwa kulitegemea sana Jeshi la Israel.”

Mwandishi huyo anaandika kuwa baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Uganda, baadaye “…fungate lao lilidumu kwa muda mfupi sana. Idi Amin alikaa na washauri wa Kiyahudi hadi Aprili 1972, kisha akawataka waondoke Uganda. Hadi hapo Amin alikuwa akishawishiwa na kushawishika zaidi na Libya na Waarabu … alitawala kwa miaka minane na hatimaye akapata hifadhi ya kisiasa kwa Waarabu.”

Katika ukurasa wa 16 wa kitabu chake, ‘Entebbe: The Most Daring Raid of Israel’s Special Forces’, mwandishi Simon Dunstan ameandika kuwa Septemba 1972 Amin aliipiga marufuku jumuiya ya Kiyahudi iliyoitwa ‘Abayudaya’. Alisema jumuiya hiyo ni haramu na mahekalu yao yakafungwa.

Msingi wa neno ‘Abayudaya’ ni lugha ya Kiganda. Kwa mujibu wa kitabu ‘The Garland Handbook of African Music’ (uk. 314) kilichohaririwa na Ruth M. Stone, msingi wa neno hilo ni ‘yudaya’ likimaanisha ‘Myahudi’. Wingi wake ni ‘Abayudaya’ likimaanisha ‘Wayahudi’.

Jumuiya hiyo ilianzishwa na mwanadamu muhimu sana katika historia ya Uganda aliyeitwa Semei Lwakilenzi Kakungulu. Huyu alikuwa ni kiongozi wa kijeshi wa Uganda aliyefanya kazi na wakoloni wa Kiingereza katika miaka ya 1890. Kwa hiyo ‘Abayudaya’ ni “Wayahudi wa Uganda” lakini sasa Idi Amin alipiga marufuku jumuiya yao na kufunga mahekalu yao.

Hata hivyo, huyu Semei Kakungulu hakuwa hai wakati Idi Amin anapiga marufuku kile alichoanzisha. Waandishi Philip Briggs na Andrew Roberts katika ukurasa wa 13 wa kitabu chao, ‘Uganda’, wanaandika kuwa alifariki Jumamosi ya Novemba 24, 1928 kutokana na homa ya mapafu. Mjukuu wake, Isaak Kakungulu, akapokea kijiti na kukiendeleza hadi Idi Amin alipokuja.

Jumanne ya Februari 29, 1972 Idi Amin alitishia kuufunga Ubalozi wa Israel nchini Uganda. Lakini balozi wa Israel ambaye alikuwa wa mwisho nchini Uganda, Daniel Laor, aliingia katika mazungumzo na Serikali ya Uganda. Hii ni baada ya kunyimwa zana za kivita alizohitaji kutoka Israel tangu Julai 1971.

Kwa mujibu wa kitabu ‘Idi Amin Dada: Hitler in Africa’ (uk. 59) kilichoandikwa na waandishi, Thomas Patrick Melady na Margaret Badum Melady—(Jumatano ya) Machi 22, 1972, Idi Amin alitangaza kuwa hatahuisha mkataba wa aina yoyote kati ya Serikali yake na Israel. Balozi Laor alionyesha kushangazwa sana na kile alichokiita kuwa ni “kigeugeu cha Baba Mkubwa”—akimaanisha Idi Amin.

Alhamisi ya Machi 23, 1972 Idi Amin akatoa amri ya kuwafukuza raia wa Israel waliokuwa Uganda na kuwapa siku tano tu za kufungasha na siku ya mwisho kuondoka ni Jumanne ya Machi 28, 1972.

Jumamosi ya Aprili 8, 1972 ndipo Ubalozi wa Israel mjini Kampala ukafungwa rasmi na hiyo ndiyo ikawa ni siku ambayo Mwisraeli wa mwisho nchini Uganda alipoondoka, akiwamo Balozi Daniel Laor mwenyewe. Kwa vielelezo hivyo, hadi Israel wanaivamia Entebbe mwaka 1976, uhusiano kati ya Israel na Uganda ulikuwa umezorota kupindukia.

Hiyo ni sehemu ya mikwaruzano iliyokuwako kati ya Israel, Wayahudi na Serikali ya Idi Amin. Kwa hiyo katika mazungumzo yake na Bar-Lev ambaye walifahamiana vyema, alisema mwishoni kabla Idi Amin hajakata simu alianza kuzungumza kikakamavu, “Si kama mwanasiasa, lakini kama askari aliyebobea kwenye kazi yake. (Idi Amin) alisema, lazima nikuambie ukweli kwamba kazi iliyofanywa na makomandoo wenu ilikuwa nzuri sana na makomandoo walikuwa bora kabisa.”

Ulipofika mchana wa siku hiyo inaelekea Idi Amin alikuwa na wazo jingine. Akaamua kumpigia tena Bar-Lev akimwomba amfanyie mpango ili Jeshi la Israel (IDF) lilipatie jeshi lake “vipuri”. Alimwambia Bar-Lev kuwa baadhi ya zana za kijeshi alizokuwa nazo hazikuwa katika ubora wake. Katika mazungumzo hayo ya mchana, Bar-Lev aligundua kuwa Urusi haikufurahishwa na ndege zao za kijeshi zilivyoteketezwa mjini Entebbe usiku wa kuamkia siku hiyo.

Itaendelea kesho…

Source: mwananchi