VIDEO: Madereva wa zamani wa DC Kilolo wazungumzia vituko vya bosi wao

0
58
By Godfrey Kahango, Mwananchi [email protected]

Iringa. Baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdalah kunyooshewa kidole na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akidaiwa kutumia vibaya madaraka yake, madereva wake wawili wa zamani wamemuelezea kiongozi huyo.

Septemba 27, Majaliwa akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Kilolo, bila kumuonea aibu, alimsema Asia hadharani kuwa anatumia madaraka yake vibaya na hana uhusiano mzuri na watumishi wa ofisi yake.

Alisema tangu ateuliwe mwaka 2016 watumishi 14 wakiwamo madereva 10 wamehamishwa vituo vya kazi na wengine aliwafukuza au kuwaweka ndani na hata waliopo hawana raha na wanaomba kuhamishwa.

Mmoja wa madereva hao (jina tunalo) aliyewahi kumuendesha Asia kwa mwaka mmoja alisema mkuu huyo wa wilaya hana staha katika matamshi kwa wasaidizi wake ikiwamo kutoa lugha chafu, pia hana uhusiano mzuri na watu wengi. “Unajua taratibu za kiongozi yeyote zinajulikana, asubuhi mnapeana taratibu za kazi, lakini unakwenda kwa kiongozi, anaingia kwenye gari bila kukupa utaratibu wowote, hasemi mnakwenda wapi,” alisema dereva huyo.

“Haya unakwenda ofisini kwake hakupi utaratibu wowote wa kazi na kama mnasafari hakuambii mnapoenda, ukimuuliza akipenda anakujibu mkato, muda mwingine hakujibu,” alisema dereva huyo ambayo sasa yupo ofisi nyingine ya serikali.

Dereva huyo alisema “sasa hapo unakuwa huelewi lolote. Kukutolea lugha chafu kwake si kesi na hata akiwa kwenye gari na watu wengine kukutusi kwake ni kawaida.”

Advertisement

Alisema kwa muda aliomuendesha Asia alifanya kazi kwa uvumilivu na kumchukulia kama alivyo na hakuwa na uwezo wa kumfanya lolote kwani alikuwa bosi wake.

“Hana mawasiliano na dereva, muda wowote unatakiwa uwe ‘standby’, ninachojua unatakiwa uandaliwe ili ujiweke sawa, lakini unaweza kumpeleka nyumbani kwake akifika tu anashuka na kwenda ndani hata neno ahsante kwa dereva hakuna.

Alisema tangu aanze kuendesha viongozi wa kiserikali amewaendesha wakuu wa wilaya wanne kwa vipindi vinne tofauti hakuwahi kukorofishana wala kutofautiana kwa lolote na hadi sasa wapo hai wanakutana na wamekuwa kama ndugu.

Dereva mwingine ambaye pia tunamhifadhi jina alisema “kuwa na kiongozi kama yule ni mateso, bora uache kazi utakuwa huru. Haiwezekani kila muda unakuwa kama mtumwa, kutukanwa ni kawaida. Hadi dereva mwenzetu mmoja alichapwa makofi, sasa mtu mzima na familia yako unaaga unakwenda kazini halafu familia inasikia baba kachapwa makofi?’

Alisema kitendo cha kuondolewa ofisini kwake na kupelekwa taasisi nyingine alifurahi na sasa anafanya kazi kwa uhuru kama mtumishi mwajiriwa anatambua wajibu na majukumu yake kwa mkuu wake wa kazi.

Alipofuatwa jana kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya wazee duniani ambayo kimkoa yalifanyikia viwanja vya Kichangani-Kihesa, Iringa, ili kuzungumza hayo, Asia alijibu kwa maneno machache. “Si mmeshaandika? Sasa mnataka niseme nini? Nyie mmeshaandika na endeleeni kuandika mnachojisikia,’’ alisema huku akiingia kwenye gari lake na kuondoka eneo hilo.

Source: mwananchi