Vigogo polisi kizimbani kwa madai ya kuomba rushwa ya Sh200 milioni

0
37
By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Maofisa upelelezi watatu wa polisi kituo cha Kawe wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu wakikabiliwa na mashtaka tisa likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kupokea zaidi ya Sh15 milioni.

Washtakiwa hao ni Shaban Shillah, Joyce Kita, Ulimwengu Rashid na Emmanuel Njegele ambaye hakuwepo mahakamani na hivyo kutolewa hati ya kukamatwa.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile mwendesha mashtaka wa Takukuru, Maghela Ndimbo, amedai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la kushawishi na kupokea rushwa, kughushi nyaraka za uongo na kutotii amri ya halali ya ofisa wa Takukuru.

Wakili Ndimbo amedai katika shtaka la kwanza washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa  Desemba 17, 2018 eneo la Social Club Rainbow Kinondoni walishawishi rushwa ya Sh200 milioni kutoka kwa Diana Naivasha  wakidai  amekamatwa na nyara za Serikali ili kushawishi hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yake.

Katika kosa jingine la kujihusisha na miamala ya rushwa kwa pamoja wanadaiwa Desemba 17, 2018 katika kituo cha polisi Kawe jijini Dar es Salaam waliomba rushwa ya Sh6 milioni kutoka kwa Diana kama kishawishi kumsaidia asichukuliwe hatua za kisheria baada ya kukamatwa na nyara za Serikali.

Katika kosa la nne, tano na sita ya kujihusisha na rushwa inadaiwa walilitenda Desemba 19, 23 mwaka 2018 na Januari 3, 2019.

Advertisement

Inadaiwa wakiwa kituo cha polisi Kawe na sehemu ya chakula kama waajiriwa katika nafasi zao walipokea  Sh2 milioni kutoka kwa Diana kama kishawishi cha rushwa kwa madai anajihusika na nyara za Serikali.

Katika kosa la kughushi nyaraka linalomkabili Joyce, anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 2018 na Aprili 3, 2019 katika maeneo ya Kinondoni akiwa mwajiriwa wa polisi.

Anadaiwa kufanya hivyo  kwa lengo la kudanganya, kutengeneza nyaraka za uongo kwa jina la Diana akidai nyaraka hizo ni za kweli na zimewekwa sahihi na Diana wakati wakijua si kweli.

Katika kosa la kutotii amri halali ya ofisa wa Uchunguzi wa Takukuru, inadaiwa Aprili 2019 wakiwa Kinondoni kwa pamoja walishindwa kutii amri halali ya kukamatwa ambayo ilitolewa na mpelelezi wa Takukuru, Colman Lubisi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washitakiwa walikana makosa yao na wakili Ndimbo kudai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia hawana pingamizi na dhamana, kuomba hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa wa nne, Njegele.

Washtakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana isipokuwa mshtakiwa Shillah na kesi hiyo kuahirishwa hadi Oktoba 16, 2019.

Source: mwananchi