Akina Tibaijuka wamsubiri DPP kurejesha Sh1.67 bilioni

0
32
By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Profesa Anna Tibaijuka amesema bodi ya wadhamini ya Shule ya Sekondari Barbro Johansson imemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ukiomba kurejesha mgao wa Sh1.67 bilioni ilizopokea kutoka kwa mfanyabiashara, James Rugemalira.

Rugemalira, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya VIP Engineering iliyohusika katika sakata la Escrow, anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi pamoja na Harbinder Seth, ambaye kampuni yake ya PAP iliinunua VIP.

Wawili hao wanahusishwa na uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka akaunti hiyo ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT) na sehemu ya fedha hizo kuonekana zikiingia kwenye akaunti za majaji, viongozi wa dini, watumishi wa umma na wanasiasa, akiwemo Tibaijuka, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Na uamuzi wa bodi hiyo unatokana na msamaha ambao Rais John Magufuli aliutangaza kwa watuhumiwa wote wa kesi za uhujumu uchumi kuwa watasamehewa iwapo watakiri makosa na kukubali kurejesha fedha kwa kiwango walichoshtakiwa.

Akizungumza na Mwananchi jana, Profesa Tibaijuka alisema hatua ya bodi hiyo inalenga kutatua changamoto iliyoko mbele yao na kwamba chombo hicho cha shule kinapaswa kujipanga upya kuhimili mtikisiko wa fedha utakaosababishwa na kurejesha fedha hizo walizopata kama msaada mitano iliyopita.

Mbunge huyo wa Muleba Kusini (CCM) alikuwa akifafanua kauli aliyoitoa juzi kupitia kituo cha televisheni cha UTV kuwa bodi ya shule imeamua kurejesha fedha ili kumsaidia Rugemalira ambaye yupo gerezani kwa zaidi ya siku 820.

Advertisement

“Tayari mwenyekiti wa bodi ya wadhamini, Balozi Salomon Odunga amemwandikia barua DPP kuhusu kurejesha fedha hizo– Sh1.67 bilioni –na sasa tunasubiri maelekezo ya DPP jinsi ya kuzirejesha,” aliliambia Mwananchi jana.

Kuhusu fedha hizo, Profesa Tibaijuka alisema walipokea msaada huo kwa nia njema na ulitumika kulipia mkopo wa majengo ya shule hiyo iliyopo eneo la Luguluni, Mbezi jijini Dar es Salaam.

“Unajua watu wanakosea, wanashindwa kutofautisha shule na mimi,” alisema Tibaijuka, mtumishi huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN).

“Fedha zilitolewa kwa shule na zikatumika kulipia mkopo na bodi ya wadhamini ya shule, imekaa kikao ambacho mimi sikuwepo– nilikuwa Marekani– na kukubaliana kuzirejesha.”

“Kama taasisi ilipokea na kuzitumia, taasisi haiwezi kushindwa kuzirejesha. Taasisi ni tofauti na mtu binafsi na ndio kama nilivyosema, tunasubiri maelekezo ya DPP.

“Watanzania huwa hawaelewi vitu vya taasisi bali watu (binafsi). Mimi ni mmoja wa waanzilishi wa shule na sio mali yangu binafsi na hiyo hela sikupewa mimi binafsi bali ilikuwa msaada kwa shule.”

Hata hivyo, wakati akitangaza mabadiliko yaliyomvua uwaziri baada ya sakata hilo, Rais Jakaya Kikwete alisema moja ya matatizo ya Tibaijuka ni fedha hizo kuingia kwenye akaunti yake binafsi na kutoweka bayana suala hilo kama kanuni za maadili zinavyotaka.

Profesa Tibaijuka alisema alichokifanya Rais kushauri watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi ni kizuri na kukifananisha na kile alichowahi kukizungumza bungeni kuwa upelelezi wa kesi za uhujumu uchumi unapaswa kufanyika haraka.

Akijibu swali la Mwananchi kuhusu hali ya shule hiyo kiuchumi baada ya kutoa fedha hizo, Profesa Tibaijuka alisema: “Ni kweli fedha ni kubwa na nyingi na ni changamoto.

“Lakini unapopata changamoto unaitatua changamoto iliyoko mbele yako. Unapozitoa (fedha) zinaacha pengo kwa kuwa ni fedha nyingi. Sh1.67 bilioni ni kubwa (hivyo) bodi itajipanga upya.”

Tibaijuka alisema fedha hizo zilitumika kulipa mkopo wa benki, lakini hiyo haimaanishi kuwa haiwezi kupata nyingine.

“Rais amesema mtuhumiwa arudishe fedha na sisi tunarejesha kile tulichokuwa tumepewa,” alisema.

Lakini pia alikuwa na maoni kuhusu wengine waliotajwa kuchukua fedha katika sakata hilo.

“Mimi nashughulika na tulichopokea sisi, siwezi kujivika uamuzi wa wengine na kila mmoja atafanya anachokiona lakini taasisi haiwezi kushindwa kulipa fedha hiyo.”

Alipoulizwa iwapo Rugemalira hatakuwa tayari kuandika barua kwa DPP kukiri kosa licha ya wao kuonyesha nia ya kurejesha fedha hizo Tibaijuka alisema “sisi tunasubiri maelekezo ya DPP na ndiye aliyepewa maelekezo, atatupa”.

Profesa Tibaijuka alisema shule hiyo imesaidiwa na watu mbalimbali na si Rugemalira pakee, akisema hata Rais wa zamani aliwapa ekari 50.”

Mbali na ubunge, Profesa Tibaijuka ni mwanaharakati wa haki za wanawake na mkulima.

“Mimi ni mbunge wa Muleba Kusini ambaye nimetangaza kung’atuka na sing’atuki kwamba nahofia kushindwa hapana, hata Mwalimu (Julius) Nyerere aling’atuka,” alisema.

“Nitaendelea kuwa mwanaharakati wa haki za kina mama na nikistaafu nitabaki kwenye jamii na yote haya yanategemea na nguvu ambazo Mungu atakuwa amenijaalia,” alisema Profesa Tibaijuka

Source: mwananchi