Majaliwa awabana watumishi Singida, awataka kurejesha fedha

0
23
By Irene Bwire, Ofisi ya Waziri Mkuu

Singida. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amempa siku tatu, Kaimu Mweka Hazina wa wilaya ya Itigi mkoani Singida, Optatus Likiliwike ahakikishe anarejesha Sh1.6 milioni ambazo alijilipa posho kinyume cha utaratibu.

“Kabla sijamaliza ziara Septemba 7,2019 nataka nione pay in slip kuthibitisha kuwa fedha hiyo imerudishwa. Adhabu yako kaweke fedha benki, niione hiyo pay in slip kabla sijaondoka,” amesema Waziri Mkuu.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Oktoba 4, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Manyoni ambao wanajumuisha Halmashauri za Wilaya za Itigi na Manyoni.

“Wewe si ndiye Otto au Optatus? Mwezi Julai ulilipwa posho ya safari ili uende Dodoma kukamilisha mahesabu ya bajeti lakini hukwenda. Taratibu za fedha zinasema ukitumia fedha, urejeshe, wewe ulifanyaje?,” alihoji  Waziri Mkuu.

“Nilichukua fedha lakini kutokana na majukumu mengi niliyo nayo, sikwenda nikawa naenda wikiendi na kuna kazi nyingine haikuwa ni lazima niwepo Dodoma,” alijibu Likiliwike.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka ofisa huyo arejeshe Sh196 milioni za ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambazo zimetumika kinyume na zilivyopangwa.

Advertisement

“Hizi fedha zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi. Hizi ni fedha za retention, ni nani alikiuka maelekezo na kuamua kuzitumia kwa kazi nyingine?” Waziri Mkuu alijibiwa kwamba ni Mkurugenzi na Mweka hazina waliokuwepo kabla yake.

Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, John Mgalula ambaye aliteuliwa wiki iliyopita asimamie marejesho ya posho za Likiliwike pamoja na marejesho ya Sh196 milioni ambazo mweka hazina huyo ameahidi kuwa Halmashauri yake imetenga Sh70 milioni ili zirejeshwe kila mwaka.

Waziri Mkuu amesema wanapaswa kutenga fedha zaidi ili fedha hiyo iweze kurejeshwa haraka kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye ni mkandarasi wa jengo la ofisi za Halmashauri hiyo.

Naye  Optatus Otto Likiliwike alisema fedha zinazodaiwa kutumika zilikuwa zimetumwa na Hazina kwa ajili ya ujenzi wa ofisi lakini zililazimika kuchotwa na uongozi uliopita ili zitumike kuweka miundombinu ya kuanzisha Halmashauri mpya ya Itigi.

Alisema waliohusika ukiukwaji huo ni Mkurugenzi aliyepita, Pius Luhende na Mweka Hazina aliyepita Charles Mnamba. Hata hivyo, alikiri fedha hizo hazikuombewa kibali cha matumizi hayo.

Akiweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo, Waziri Mkuu alisema anaweka jiwe hilo kwa sababu ameridhishwa na maelezo ya Meneja wa TBA kuhusu ujenzi wa jengo hilo.

Amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo wahoji matumizi ya fedha hizo na wawaorodheshe wote waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo. “Kaeni na mkaguzi wenu wa ndani, awape taarifa juu ya matumizi hayo,” alisema.

Pia amewataka watumishi wa umma waheshimiane na watambue mamlaka nyingine kama za madiwani. Pia, aliwataka wafuate taratibu na kanuni za utumishi na siyo wajifanyie mambo kwa holela.

Awali, Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Charles Fussi ahakikishe anarejesha mkopo wa Sh100 milioni kutoka benki ya CRDB ambazo walikopeshwa madiwani, wakarejesha kiasi lakini Halmashauri haijazipeleka benki.

Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa deni hilo kutokana na malimbikizo ya muda mrefu na riba zinazotozwa na benki.

“Hakikisha unamaliza hilo deni la sivyo hawa waheshimiwa hawatapata stahili zao hadi deni liishe. Pia unataka kusababisha mgogoro baina ya benki na Halmashauri.”

Aliwataka madiwani hao waisimamie kwa karibu Halmashauri yao. “Madiwani muiangalie Halmashauri yenu kwa kina. Hatuwezi kuendesha Halmashauri kwa utaratibu huu wa kila mmoja kufanya kazi anavyotaka.”

Source: mwananchi