Makonda aomba taasisi, kampuni kuchangia matibabu

0
32
By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewataka watu, kampuni na taasisi mbalimbali kuendelea kuchangia kufanikisha matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto wanaohitaji huduma hiyo.

Makonda ameyasema hayo leo alipowatembea watoto wanaosubiri kufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akiwa sambamba na Mkurugenzi wa kampuni ya mafuta Puma Energy Tanzania Dominic Dhanah.

Septemba 30, 2019 kampuni hiyo ilitoa Sh40 milioni kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya moyo kwa watoto 20 kati ya 500 wanaohitaji kufanyiwa upasuaji moyo kazi itakayofanyika kaunzia Oktoba 7 mwaka huu.

Makonda amesema uwepo wa watu wengi watakaoguswa kuwasaidia watoto hao utasaidia kurudisha tabasamu kwa familia za watoto hao zilizokata tamaa kutokana na kuuguza kwa muda mrefu.

Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema  uwepo wa taasisi hiyo  umesaidia kupunguza gharama za matibabu yanayohusiana na upasuaji wa moyo ikilinganishwa na hapo awali huduma hiyo ilikuwa ikipatikana India kwa Sh30 milioni kwa mgonjwa mmoja.

“Kwa wagonjwa 200 tuowafanyia upasuaji ingetugharimu zaidi ya Sh9.4 bilioni lakini itagharimu Sh400 milioni. Hawa watoto mnaowaona hapa wamechangamka baada ya kufanyiwa upasuaji, walipokuja walikuwa wanyonge kwa sababu ya maumivu waliyokuwa nayo,”

Advertisement

Kwa upande wake Dhanah amepongeza juhudi zinazofanywa na JKCI katika kuokoa maisha ya watanzania na watoto wenye matatizo ya moyo ambao tayari walishapoteza matumaini lakini kupitia taasisi hiyo wamerudisha matumaini ya kuishi.

 “Mnafanya kazi kubwa ya kurudisha maisha yaliyokuwa hatarini kupotea, vilevile ninampongeza mkuu wa mkoa kwa  kusimamia hili kwa umakini. Tunafahamu wazazi wa watoto hawa hakuwa na fedha za kugharamia matibabu haya lakini Puma Energy tutaendelea kuunga mkono hatua kwa hatua,” amesema Dhanah

 Ameongeza kuwa wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kusaidia watu wenye mahitaji kama yalivyo kwa watoto hao ambao wapo katika taasisi hiyo lakini wanatoka katika mikoa karibu yote nchini Tanzania.

Source: mwananchi