MIAKA 20 BILA NYERERE: Mwalimu Nyerere awa waziri mkuu kwa siku 266 tu -2

0
39
By William Shao

Baada ya Chama cha Tanu (Tanganyika African National Union) kushinda katika uchaguzi na kupata idadi kubwa ya wajumbe katika Baraza la Kutunga Sheria (Legco au Tanganyika Legislative Council), Mwalimu Julius Nyerere aliteuliwa na Gavana Richard Gordon Turnbull kushika wadhifa wa waziri kiongozi (chief minister). Nyerere alianza kuutumikia wadhifa huo kuanzia Ijumaa ya Septemba 2, 1960 na alidumu katika wadhifa huo kwa siku 241 hadi cheo kilipopanda tena.

Alipanda cheo na kuwa waziri mkuu kuanzia Jumatatu ya Mei Mei, 1961. Hiyo ndiyo siku aliyoapishwa kuwa waziri mkuu baada ya Tanganyika kupewa serikali ya mambo ya ndani (Internal Self Government) kabla ya uhuru kamili. Hata hivyo, Jumatatu Januari 22, 1962 Nyerere alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu.

Kwa vipindi tofauti mwaka 1955 na 1956, Nyerere alikwenda New York, Marekani, kuhutubia Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa Tanganyika. Mwaka baadaye, 1957, alitangaza kuwa Tanu ingeshiriki uchaguzi mwaka 1958 ikiwa tu ungekuwa uhuru na wa haki. Serikali ya kikoloni iliuhakikishia Umoja wa Mataifa kuwa uchaguzi huo utakuwa huru. Huo ndio ulikuwa uchaguzi mkuu wa kwanza Tanganyika.

Kwa mujibu wa kitabu ‘Elections in Africa: A Data Handbook’ © 1999, uchaguzi wa kuwapata wabunge ulifanyika Jumatatu Septemba 8 na Ijumaa ya Septemba 12, 1958. Mwaka uliofuata uchaguzi wa majimbo yaliyobakia ukafanyika Jumatatu ya Februari 9 na Jumapili ya Februari 15, 1959, kisha ukafanyika mwingine Jumanne ya Agosti 30, 1960.

Jarida la ‘Black World/Negro Digest’ la Machi 1962 liliripoti kuwa katika uchaguzi wa 1958, wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 885,000. Hadi mwishoni mwa Julai, wagombea 58 wa Tanu walipita bila kupingwa na 39 miongoni mwa hao ni Waafrika.

Tanu ilipata viti 12 kati ya 13 vilivyogombewa katika Baraza la Kutunga Sheria. Mgombea mmoja wa Tanu, Chief Amri Dodo alishindwa na mgombea binafsi aliyeitwa Herman Elias Sarwatt katika jimbo la Mbulu.

Advertisement

Katika hotuba yake ya Mei Mosi 1995 katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, Nyerere alikiri: “Sasa, mfano mmoja ninaoutumia mwisho kabisa kabisa, mwaka 1970 sijui 1971 sijui 1972, eeh! Akatupinga kijana wetu mmoja anaitwa Sarawati katika uchaguzi wa vyama vingi.

“Ulikuwa uchaguzi wa vyama vingi eeh? Ndiyo. Ilikuwa uchaguzi wa vyama vingi. Ilikuwa ni katika uchaguzi wa vyama vingi. Viti vingi sana tulivichukua bila kupingwa. Nadhani hivyo ndivyo ilivyokuwa.

“Katika kiti cha Mbulu tumemweka mtu mmoja anaitwa Chifu (Amri) Dodo. Mwanachama wetu mmoja pale anaitwa Herman Sarawati akasema aaah, hiki chama changu hakina akili hata kidogo. Au viongozi wangu hawana akili…Huyu akiwa na mkoloni ndiye aliyetaka kutufunga sisi ndiye wameonelea awe mbunge wetu katika Jimbo la Mbulu?

“Kijana yule akatupinga. Mimi nikatoka Mbeya. Nimesafiri kutoka Mbeya hapa kwenda kumpinga. Kwenda kumtetea yule candidate (mgombea) wa Tanu nikashindwa. Wananchi wa Mbulu na wanachama wengi tu, wakasema Tanu wamekosea. Wakampa kura Sarawati. Mwanachama wa Tanu wakafanya hivyo.

“Anasimama mwenyewe tu. Akatupinga. Ilikuwa haki yake. Mimi nilidhani sasa tunarudisha vyama vingi, tunarudisha na haki zote zile zilizokuwapo za raia, pamoja na haki, si haki ya kuunda vyama tu pamoja na haki ya private candidate (mgombea binafsi) kusimama akafanya kama chama kinavyofanya.”

Kutokana na ushindi wa Tanu katika uchaguzi wa Septemba 1960, Nyerere akawa waziri kiongozi wa Tanganyika, akamteua Derek Bryceson kuwa makamu wake. Serikali ya kikoloni iliweka masharti kadhaa kwa wale ambao wangekuwa wapiga kura katika uchaguzi huo wa 1958. Mojawapo ni lile la kuwataka wapigakura kuwapigia kura (tatu) kutoka kundi la Waafrika, Wahindi na Wazungu.

Legco iliyoundwa na Waingereza tangu mwaka 1926, ilikusudiwa kuwajumuisha Wazungu, Wahindi na Waafrika. Vyama vingine vya siasa vilivyoshindana na Tanu katika uchaguzi huo ni Tanganyika United Party (UTP). Hiki kilikuwa chama cha walowezi lakini kiliungwa mkono na Wahindi wachache na baadhi ya Waafrika.

Kwa kuona utata wa masharti yaliyowekwa na wakoloni kuhusu uchaguzi huo, Tanu iliitisha mkutano wake wa mwaka uliofanyika Tabora kuanzia Januari 21 hadi 26, 1958, ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi huo. Ajenda kuu ilihusu uchaguzi huo. Mkutano huo uliitwa kutafakari juu ya ama kushiriki au kuususia uchaguzi.

Masharti mengine ambayo Waingereza waliyaweka ni kwamba ili upige kura lazima kwanza uthibitishe una kipato cha pauni 400 za Uingereza kwa mwaka, uwe na elimu isiyopungua darasa la 12 na ajira ya muda wote ambayo inathibitishwa na serikali ya kikoloni. Masharti yote haya na mengine yalikuwa na lengo la kuwazuia Waafrika wengi kupiga kura katika uchaguzi huo. Kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo kuliwagonganisha sana wajumbe wa mkutano. Hali hiyo iliwafanya wajumbe hao wa Tanu na hivyo kugawanyika makundi mawili, kundi la kwanza likisisitiza chama kishiriki, la pili likitaka kuususia.

Mmoja wa waliosisitiza kuususia uchaguzi huo ni Sheikh Suleiman Takadir, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Tanu, na mwingine ni Zuberi Mtemvu, katibu mwenezi wa Tanu. Hawa walikaribia kabisa kukipasua chama na walielekea kufanikiwa kama Nyerere asingeingilia kati kuwashawishi wakubali chama kishiriki uchaguzi.

Ubishani wa Nyerere na Sheikh Takadir kuhusu kushiriki au kutoshiriki uchaguzi ulizidi hadi wawili hao kufikia mahali pa kutoelewana. Matokeo ya hilo Sheikh Takadir alivuliwa uanachama wa Tanu.

Wengine waliopinga vikali Tanu kushiriki uchaguzi huo ni Jumanne Abdallah na Bhoke Munanka. Lakini baada ya siku kadhaa za malumbano makali, Nyerere aliungwa mkono na wengi wakiwamo Abdallah Rashidi Sembe, Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Ng’azi Mohammed, Mustafa Shauri na Abdallah Makata waliokuwa viongozi wa Tanu kutoka Tanga.

Mkutano huo ulitoa tamko kuwa endapo Serikali ya kikoloni haitahakikisha Tanganyika inapewa uhuru bila kuchelewa, Tanu ingewahamasisha wananchi wote wagome. Kwa kauli moja tamko hilo likaitwa “Positive Action”. Pia mkutano huo uliazimia kupinga pendekezo la serikali ya kikoloni la kuitaka Tanu ikubali mpango wa kila mpigakura awapigie watu watatu; Mzungu, Mhindi na Mwafrika ili kushindana na chama kingine cha siasa cha UTP kilichokuwa na matajiri wa Kizungu na Kihindi.

Tanu iliibuka na ushindi baada ya kupata viti 28 kati ya 30 vilivyokuwa vinagombewa. Miaka miwili baadaye, ulipofanyika uchaguzi wa wabunge, Tanu ilipata viti 70 kati ya 71 vilivyogombewa. Kutokana na ushindi huo, Rais wa Tanu, Mwalimu Julius Nyerere, akateuliwa kuwa waziri kiongozi wa Tanganyika Ijumaa ya Septemba 2, 1960. Hata hivyo alidumu katika wadhifa huo kwa siku 241 hadi alipoteuliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika Jumatatu ya Mei Mosi, 1961.

Hata hivyo, Jumatatu ya Januari 22, 1962 Nyerere alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu ikiwa ni miezi minane baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu? Ni kweli alijiuzulu kwenda kukijenga chama cha Tanu kama ilivyodaiwa?

Source: mwananchi