Idadi wagonjwa wa akili yaongezeka Muhimbili

0
21
By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Matatizo ya akili ni miongoni mwa maradhi yanayowsumbua wengi nchini hata duniani.

Ripoti ya Shirikisho la Afya ya Akili Duniani (WFMH) ya mwaka 2017 inaonyesha mtu mmoja kati ya wanne ana matatizo ya akili huku katika maeneo ya kazi ni mtu mmoja kati ya watano.

Kutokana na idadi hiyo, gharama za kuwahudumia wagonjwa hao inatarajiwa kuongezeka na kufika Dola 6 trilioni za Marekani mwaka 2030 kutoka Dola 2.5 trilioni zinazotumika sasa.

Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), muuguzi msaidizi, Sofia Sanga idadi ya wagonjwa wanaopokelewa sasa imeongezeka kidogo tofauti na zamani.

Zamani, anasema walikuwa wanapokea kati ya wagonjwa wapya wawili hadi watatu kwa siku lakini sasa wanafika mpaka 20.

“Hata kliniki ilikuwa unaweza kuwaona wagonjwa 20 hadi 30 kwa siku ila sasa idadi hiyo imeongezeka zaidi,” anasema Sofia.

Advertisement

Ongezeko hilo, anasema huenda wagonjwa wengi walikuwa mtaani bila kupelekwa hospitalini. Ingawa idadi ya wagonjwa wanaopokelewa inaongezeka, anasema bado jamii haijapata elimu ya kutosha kuhusu magonjwa ya akili hivyo wengi kuendelea kubaki nao nyumbani.

Wengi wanaougua na waliolazwa wodini anasema wana kati ya miaka 17 na 40 ambao ni umri wa kujitegemea kimaisha hivyo kuwa ni kipindi cha kukutana na changamoto nyingi za maisha.

Kutokana na jamii kukosa elimu ya kina kuhusu maradhi haya, wengi huamini katika ushirikina kuwa chanzo cha magonjwa ya akili. Wachache huyahusisha na malaria iliyopanda kichwani.

“Wakifika hospitali, daktari akimuangalia anaona hakuna maralia iliyopanda kichwani. Anapewa rufaa kuja hapa. Tunawapata wengi kwa staili hii,” anasema Sofia akieleza jinsi wanavyowapokea wagonjwa.

Wengine, anasema hupelekwa na ndugu zao na wapo wanaotolewa wodi za kawaida kupelekwa katika kitengo hicho cha afya ya akili.

Kutokana na operesheni zao, anasema wapo wagonjwa wanaoletwa na askari polisi wakiwa wamekamatwa kutokana na tuhuma tofauti.

“Wapo wanaokuja wakiwa wamefungwa kamba kutokana na vurugu wanazofanya,” anasema.

Kwa sasa Muhimbili hupokea wastani wa wagonjwa 15 kwa siku huku zaidi ya 100 wakihudhuria kliniki baada ya kuruhusiwa kutoka wodini.

“Hawa ambao wako kliniki idadi yao hutegemeana kanda wanayotoka. Tuna kanda ya Magomeni, Ilala, Kinondoni na Temeke hivyo idadi huweza kuwa zaidi au pungufu kidogo,” anasema.

Kwa mikoani, anasema wapo wengi na walio karibu na Dodoma hupelekwa Milembe kwa matibabu hayo.

Sofia anasema kuna sababu nyingi za magonjwa haya ambazo jamii inapaswa kuelimishwa ili kuchukua hatua stahiki kila inapobidi ikiwamo kuwafikisha wagonjwa husika hospitalini mapema pindi wanapoona dalili.

Hiyo ni kutokana na jamii kuendelea kuwa na dhana ya kuwa magonjwa ya akili hutokana na kurogwa jambo ambalo hufanya asilimia kubwa ya waathirika kutopata matibabu.

Kwa kuwa afya ya akili ndiyo humfanya mtu kuwa na uamuzi sahihi katika mambo mbalimbali, anasema ipo haja ya kuwasaidia wagonjwa ili nao wafanikishe mambo yao na kuepuka vitu hatarishi wanavyoweza kufanya kwa kutotibiwa.

“Kuna sababu nyingi za magonjwa ya akili. Wapo wanaorithi kutoka kwa ndugu zao, wengine ni kutokana na maradhi mengine,” anasema Sofia.

Kwa mzazi aliyewahi kuugua maradhi haya, upo uwezekano wa mmoja wa watoto wake au mjukuu na hata kitukuu kuupata.

Wapo baadhi ya watu wanaoweza kuishi na vinasaba vya kurithi vya ugonjwa huo lakini visionekane kama hakuna visababishi vya kumfanya awe mgonjwa.

“Inawezekana ukoo fulani una matatizo ya ugonjwa huu lakini siyo lazima kila mtu aumwe isipokuwa kama atafanya vitu vitakavyochochea mfano kuvuta bangi,” anasema.

Sababu nyingine ya kupata maradhi haya ni changamoto za maisha hasa linapojitokeza jambo ambalo mtu anashindwa kulitatua. Wanaotumia dawa za kulevya au wanaougua Ukimwi na hawatumii dawa pia wapo kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa akili.

Msongo wa mawazo unaosababishwa na kitu chochote endapo utadumu kwa muda mrefu nao unaweza kusababisha ugonjwa wa akili.

Kufyatuka kwa akili au schizophrenia ni sababu nyingine inayowaingiza wengi kwenye matatizo ya aafya ya akili. Sofia anasema wagonjwa anaowahoji huitaja sababu hiyo.

Schizophrenia ni hali ya akili kugawanyika au kutawanyika, yaani kukosa muunganiko. Mtu anayekuwa katika hali hii akili huwa haitulii kwani anaweza kuwa anasikia kelele ayeye peke yake, akatoa kauli kusema vitu visivyoeleweka au kuchelewa kuelewa vitu.

Anayeugua tatizo hili hukosa muunganiko wa matukio na hali halisi ya maisha yake kwani kuna wakati huwa katika hali ya kawaida na wakati mwingine hufanya vitu vinavyoshangaza wengi.

Huduma kwa wagonjwa

Kuna namna mbili za kuwahudumia wagonjwa wa akili, anasema Sofia. Mosi ni kuwapa ushauri kama hali zao si mbaya sana na pili ni kuwatibu kwa dawa.

Kuchagua namna ya kumhudumia, anasema hutegemea hali ya mgonjwa kwani mwenye fujo, anayeongea vitu visivyoeleweka huhitaji dawa lakini wapo wanaoweza kujieleza hivyo kuhitaji kuelimishwa maeneo machache yanayowasumbua.

Kwa anayejieleza, anasema “Kama atahitaji dawa atapewa na akihitaji kukutana na mwanasaikolojia atakutanishwa naye ila atawekwa kwenye muendelezo wa kliniki zetu kufuatilia maendeleo yake,” anasema Sofia.

Kwa wanaopewa dawa, wapo wanaoruhusiwa kurudi nyumbani lakini wengine hulazwa hasa walio katika hali mbaya kwa mfano mgonjwa anayezungumza habari za kujiua au kupiga watu.

Anayetaka kujiua, anasema mtu huyo huonekana kuwa si hatarishi kwa wengine lakini ni anahatarisha afya yake mwenyewe.

Wapo baadhi ya wagonjwa ambao ni hatari kwa jamii hivyo wakikaa nyumbani wanatishia kupiga watu, kubaka au wengine wameshafanya hivyo ni lazima wawekwe chini ya uangalizi na matibabu.

“Baada ya matibabu, akionekana kuwa sawa, anaruhusiwa kwenda nyumbani kuendelea na dawa kwa kufuata utaratibu wa kliniki huku ndugu zake wakimsimamia,” anasema muuguzi huyo.

Ili kukabiliana na matatizo ya ugonjwa huo, Sofia anashauri jamii ielimishwe hasa ikiwamo kuwashauri kuacha kutumia vilevi, bangi na dawa nyingine za kulevya.

Pia, watu wenye maradhi mbalimbali ikiwemo Virusi Vya Ukimwi wanapaswa kuzingatia matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo.

Source: mwananchi