Uchomaji moto makanisa, misikiti wamkera Askofu Msonganzila

0
32
By Anthony Mayunga [email protected]

Serengeti. Vitendo vya uchomaji moto makanisa, misikiti na taasisi za shule vinavyoendelea hapa duniani, ni matokeo ya kukosa heshima na hofu ya Mungu.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma nchini Tanzania, Michael Msonganzila ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 5, 2019 alipokuwa akihubiri kwenye Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa Katoliki la Mugumu mkoani Mara.

Amesema hali hiyo inawatia hofu waamini wa Kikristo na Kiislamu duniani kote.

“Nani anawatuma hawa, nani yuko kwenye hujuma hii  asiye na hofu  ya Mungu, mashambulizi haya ni kila kona mpaka Marekani,” amesema Askofu Msongazila.

Amesema Ukristo unatoa huduma kwa watu wanaohudumiwa na Serikali, kwa nini wafanyiwe hujuma kama hizo zinazolenga kurudisha nyuma huduma hiyo ambayo ndiyo kiini cha amani duniani.

“Watumishi wa umma naomba mtumikie nafasi zenu kwa uadilifu maana huo ndiyo utume mlioitiwa na Mungu kuwahudumia wananchi, kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmekamilisha hitaji la Mungu ndani mwenu,” amesema.

Advertisement

Kuhusu wanafunzi wanaoshirikiana na makundi mbalimbali kuchoma moto majengo ya taasisi za shule, amesema vitendo hivyo havitakiwi kuvumiliwa kwa kuwa vinawafanya Watanzania waendelee kuzidiwa na adui ujinga.

“Toka tumepata Uhuru tunapambana na adui ujinga tunajitahidi kujenga shule ili tumshinde, kuruhusu watoto na watu wengine watekeleze uovu huu,  tushikamane kupingana na matukio hayo,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Askofu huyo amekemea walimu wanaojihusisha na vitendo vya ngono na wanafunzi kuwa havina tofauti na wanaochoma moto majengo ya shule.

“Kuna mtindo wa ajabu wa walimu kuwapa mimba wanafunzi kisha wanawataka wawasingizie wanafunzi wenzao, imefikia hatua walimu wanajisifia, hii ni hatua mbaya sana lazima ikemewe na ndiyo kazi yetu kama Kanisa kukemea,” amesema  Askofu Msonganzila.

Awali, akisoma hati kutoka Vatican ya kuruhusu altare kutabarukiwa, katibu wa Askofu, Padri Cleophace Chacha alisema kibali hicho kinabainisha kuwa Kanisa hilo litatumika kwa Sala na si kazi nyingine.

Askofu pia amefungua nyumba ya masista iliyojengwa na waamini wa kanisa hilo na kufungisha ndoa 15.

Source: mwananchi