Kigwangalla aogopa kutumbuliwa, atoa siku 14 kwa watendaji

0
25
By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Karatu. Waziri wa  Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk Hamisi Kigwangalla amewapa siku 14 watendaji wa wizara hiyo kukamilisha mchakato wa kukamilisha sheria ya Jeshi Usu ili ifikishwe bungeni.

“Nataka mkutano ujao wa Bunge niiwasilishe sheria hii kulingana na maagizo niliyopewa na Rais John Magufuli,  sitaki kujiona nikitumbuliwa kwa sababu ya kuchelewa kutimiza wajibu wangu,” amesema Dk Kigwangalla.

Mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda katika mfumo wa Jeshi Usu, unalenga kuleta suluhisho la kudumu katika kukabiliana na changamoto za usimamizi wa rasilimali, misitu, wanyamapori na ujangili maeneo ya Hifadhi za Taifa.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 6, 2019 wakati akifunga mafunzo ya awali ya Jeshi Usu  Kozi namba Moja  ya Mwaka 2019 kwa askari 112 wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wilayani Karatu mkoani Arusha.

Dk Kigwangalla amewaagiza watendaji wakiongozwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf  Mkenda katika muda huo kukamilisha mchakato wa Sheria ya uanzishwaji wa jeshi hilo linalotumika katika ulinzi wa misitu.

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa Tanapa, Jenerali mstaafu George Waitara akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake wa bodi za uhifadhi za Tawa, TFS na Ngorongoro, aliwataka wahitimu hao kutafakari maneno ya kiapo chao.

Advertisement

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewataka wahitimu hao kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii.

Source: mwananchi