Majaliwa aagiza watumishi 48 Iramba kuchunguzwa kwa ubadhirifu

0
49
By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemwagiza kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)  Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda kuwachunguza watumishi 48 wanaodaiwa kuhusika na upotevu wa fedha.

Taarifa iliyotolewa leo Oktoba 6, 2019 na ofisi ya waziri mkuu inaeleza kuwa mtendaji mkuu huyo wa Serikali alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na  watumishi na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Iramba.

Katika mkutano huo, Majaliwa amebainisha maeneo saba yanayotakiwa kufanyiwa uchunguzi  wa kina ili kubaini upotevu huo, likiwemo eneo la upotevu wa makusanyo ya ndani kupitia mawakala wa ukusanyaji mapato.

Majaliwa ameeleza kuwa  mawakala wanaokusanya fedha wanashirikiana na watumishi wa halmashauri na kuzitumia bila kuziingiza benki.

Amesema kundi la watumishi 10 wakiongozwa na mtumishi wa idara ya Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano)  wameshirikiana kupata namba za siri,  na fedha zikishakusanywa zinatolewa na kutumika bila kuzipeleka benki.

“Wamesahau kwamba malipo yalipoingizwa mara ya kwanza, data ilirekodiwa kwenye mfumo wa malipo na sisi tunaona ni kiasi gani kimekusanywa,” amesema Majaliwa.

Advertisement

Kutokana na upotevu huo, Majaliwa ameagiza kaimu mweka hazina wa wilaya hiyo kukaa pembeni   kupisha uchunguzi wa Takukuru hadi utakapokamilika.

Amesema  mchezo mwingine uliochezwa na watumishi 38 wa halmashauri ambao walilipwa Sh46 milioni zilizokuwa sehemu ya Sh400 milioni kwa ajili ya kujenga vituo vya afya vya Ndago na Kinampanda wilayani humo.

“Hapa nina vocha zote za malipo walipeana fedha watu hawa akiwemo mkurugenzi wao. Lakini ni kazi gani ambayo kundi lote hili lilikuwa likiisimamia na kustahili kupata malipo hayo?”

“Kutoka makao makuu ya wilaya hadi Ndago au Kinampanda kuna umbali gani? Kamanda wa Takukuru fanya uchunguzi, fuatilia wote waliohusika sababu majina tunayo, kama hawastahili kulipwa ni lazima warudishe fedha yetu,” amesema Majaliwa.

Amesema fedha za walimu kiasi cha Sh29  milioni  iliyotumwa na Tamisemi  kwa ajili ya malipo ya likizo mkurugenzi alizitumia kulipia usafirishaji wa makontena ya vifaa vya tiba kutoka Sweden hadi Singida wakati mkataba wa malipo  uliuonyesha halmashauri ilipaswa kulipia kutoka bandari ya Tanga hadi Singida.

“Nataka hii fedha ya walimu  irudishwe mara moja. Pia kuna Sh6.86 milioni  ambazo mmedai ni malipo ya kukomboa mizigo bandarini wakati vifaa hivyo vilipata msamaha wa kodi.

“Kuna Sh34milioni zililetwa kurekebisha Ikama za walimu lakini hadi leo hazijalipwa. Kamanda wa Takukuru nataka uniambie nafasi ya ofisa elimu ikoje kwenye suala hili,” amesema Majaliw

Source: mwananchi