Msajili anavyoweza kumchomoa Mbowe

0
34
By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Hofu ilitanda wakati wa kupitisha marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa kuwa msajili amepewa madaraka makubwa, lakini sheria hiyo ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Huku Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikitaka maelezo ya maandishi kwa Chadema kuhusu kutofanyika kwa uchaguzi wa viongozi, hofu hiyo inaweza kutanda tena.

Barua ya ofisi ya Msajili ya Oktoba Mosi, 2019 iliyosainiwa na Sisty Nyahonza inasema uongozi wa Chadema umemaliza muda wake tangu Septemba 14, 2019, hivyo anataka maelezo kwa nini Chadema isichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka sheria hiyo, katiba na kanuni zao. Wamepewa hadi Oktoba 7, 2019 saa 9:30 alasiri wawe wamejibu.

Ibara ya 6.3.2(a) ya katiba ya Chadema inataka kila kiongozi kukaa madarakani kwa muda wa miaka mitano.

Ingawa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji anasema hawajavunja katiba na badala yake wameifuata baada ya kuahirisha uchaguzi wake mkuu kutokana na vikao vyao vya ngazi ya chini kuzuiwa na mamlaka na kwamba utafanyika ifikapo Desemba 18, 2019, bado hali inaweza kuwa tete na hasa kwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ambaye anatakiwa kuwa msimamizi wa katiba.

Kama Msajili akiridhika kuwa chama hicho kimekwenda kinyume na katiba au sheria yake, kinaweza kuadhibiwa chama chenyewe au anayekiongoza ambaye ni Mbowe.

Advertisement

“… Msajili anaweza kumfungia mwanachama yeyote wa chama cha siasa ambaye amekiuka kifungu chochote cha sheria hii kushiriki katika shughuli za kisiasa,” kinasema kifungu cha 21 (e) (1) ambacho ni kipya katika Sheria ya Vyama vya Siasa.

Na kosa linaloweza kusababisha utekelezaji wa kipengele hicho ni kama lilivyotajwa na msajili katika barua yake kwa Chadema.

“Kitendo cha Chadema kusogeza mbele uchaguzi wa viongozi wa kitaifa bila kuwa na sababu za msingi na ushahidi wa sababu husika hata kama ni za msingi, ni kukiuka sheria ya vyama vya siasa, Katiba na kanuni zenu,” inasema barua hiyo.

Pia, kifungu cha 21 (3) kinaeleza kuwa pale ambapo “Msajili ataridhika kuwa mwanachama amekiuka sheria hii, msajili atakitaka, kwa maandishi, chama chake ili kimchukulie hatua kama zilivyoelezwa kwenye katiba ya chama ndani ya siku 14”.

Na chama kikishindwa kuchukua hatua, Msajili atakiandikia pamoja na mwanachama huyo kuhusu nia yake ya kumfungia kushiriki shughuli za kisiasa.

Na mwanachama huyo akishapokea maandishi hayo, atawasiliana na Msajili au atatoa sababu zisizotosheleza, Msajili atamfungia kushiriki shughuli za kisiasa kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

Kosa jingine ni kama lilivyoandikwa katika ibara ya 7.7.9 ya Katiba ya Chadema inayotaka mikutano ya chama hicho kufanyika kila baada ya miaka mitano. Pia ibara ya 7.6.10 (a) inasema kiongozi wa Chadema “atakuwa ameshindwa kutekeleza wajibu wake, ikiwa ameshindwa kuitisha vikao vya kikatiba kwenye ngazi husika”.

Hata hivyo, wasiwasi zaidi unakuja kutokana na madaraka makubwa aliyonayo Msajili, na katika kifungu cha 4.5 (b), Msajili ana wajibu wa kusimamia chaguzi za ndani za chama na mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Hata hivyo, Chadema wanaweza kujipa nguvu kutokana na ibara ya 6.3.3 (a) ya katiba yake inayoeleza kuwa “tarehe ya uchaguzi wa chama inaweza kurekebishawa kwa kusogezwa mbele kwa muda usiozidi mwaka mmoja, toka mwisho wa uhalali wa uongozi uliopo. Mamlaka ya kufanya marekebisho haya yameachwa kwa Kamati Kuu”.

Hofu ya wafuasi wa Chadema imejikita katika kipengele hicho kwamba Msajili anaweza kutumia mamlaka yake kumfungia Mbowe kushiriki shughuli za kisiasa kutokana na makosa hayo ya kiutawala katika kipindi ambacho uchaguzi utakuwa ukifanyika na hivyo kupoteza sifa ya kutetea nafasi yake.

Wapinzani wa Mbowe, hasa walio nje ya chama hicho wamekuwa wakidai kuwa mbunge huyo wa Hai ameshika uenyekiti kwa muda mrefu na anastahili kuachia wengine kuongoza chama au kuruhusu “mawazo mapya”.

Mbowe (58), anayejulikana kama mwanamikakati na kiongozi wa sasa wa kambi ya upinzani bungeni, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chadema kwa mara ya tatu mwaka 2014 aliposhinda kwa asilimia 97 ya kura zote, akimshinda Gambaranyera Mongateo aliyepata asilimia 3 ya kura.

Alishika nafasi hiyo ya uongozi wa chama kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na mwaka uliofuata akapitishwa kugombea urais na kujipatia asilimia 5.88 ya kura zote, huku chama chake kikiongeza wabunge kutoka watano hadi 11.

Hakugombea katika uchaguzi uliofuatia, lakini mwaka 2015, akiwa na viongozi wengine wa vyama vinne vya siasa, waliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wakamteua waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea urais uliowawezesha wapinzani kupata asilimia 39.9 ya kura za urais na kuingiza karibu theluthi moja ya wabunge, Chadema ikiongoza na hivyo kushika nafasi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB), nafasi waliyo nayo hadi sasa.

Akizungumzia majukumu yake Septemba 19, 2018, Mbowe alisema japo kazi hiyo ni msalaba, lakini hawezi kuondoka kwa kuambiwa na watu wa nje.

“Hakuna faida kuwa mwenyekiti wa Chadema. Huu ni utume, hii ni kazi yenye msalaba. Nimepewa mamlaka na wana-Chadema wakitaka Mbowe aondoke kesho, naondoka tena nitashangilia. Nafanya na sherehe lakini kuambiwa na CCM ‘Mbowe ondoka’, siondoki,” alisema Mbowe.

Source: mwananchi