DED wa Mkalama matatani

0
35
By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mkalama. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama, Godfrey Sanga ameingia matatani baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kudai kuwa amekuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kutokana na makosa hayo, Waziri Mkuu alimuagiza kamanda wa Takukuru wa mkoa, Adili Elinipenda kumchunguza mkurugenzi huyo.

Baadhi ya tuhuma zinazomkabili ni kujilipa posho ya safari Machi mwaka huu bila kusafiri, kuwasainisha watumishi wa chini yake vocha na kisha kuwapa “asante kidogo” kwa madai fedha hizo zinaenda mkoani, kujilipa stahiki kabla ya wakati na kuagiza gari liende gereji kwa matengenezo bila nyaraka zozote.

“Kuna watumishi wanne uliwaambia wasaini vocha ya Sh1,320,000, hii ni kwa safari iliyopangwa kati ya tarehe 15 na 24, Septemba, mwaka huu, ukawapa asante ya Sh30,000 ukidai kuwa zinatakiwa mkoani,” alisema Majaliwa.

“RAS ni kweli hela hiyo ililetwa mkoani?”

Lakini akajibiwa na katibu tawala wa mkoa, Dk Anjelina Lutambi kwamba hakutoa hayo maagizo.

Advertisement

Alipoulizwa mweka hazina wa wilaya hiyo, Peniel Mbula kwamba fedha alilipwa nani, alijibu kwamba alikuwa Dodoma kikazi.

Mhasibu aliyekaimu nafasi yake, Lulu Hamadi aliwataja watumishi hao kuwa ni Stella Mawa, Godfrey Mnubi, Richard Laizer na Method Kafuku.

Waziri Mkuu aliwasimamisha watumishi hao na kutaka waeleze walilipwa posho hiyo ili waende wapi, lakini walikosa majibu. Ndipo akawaeleza kuwa walimkabidhi mkurugenzi na wakalipwa asante ya Sh30,000.

Alipoulizwa kuhusu malipo ya Sh1,090,000 ambayo yalilipwa Septemba 9, yalikuwa ya nini, mkurugenzi huyo alijibu kuwa ni ya stahiki zake za kila mwezi na kati ya fedha hizo, Sh600,000 ni za malipo ya nyumba Sh230,000 ni za umeme na Sh260,000 ni za simu. Lakini hakuweza kujibu ni kwa nini amejilipa kabla mwezi haujaisha.

Kuhusu gari la elimu lililopelekwa gereji kupakwa rangi kwa gharama ya Sh7 milioni, Waziri Mkuu alitaka aonyeshe dokezo lililotumika kupitisha idhini hiyo na malipo hayo, lakini akajibiwa hakuna utaratibu wa kuandika dokezo wakati magari ya halmashauri yanapoenda kufanyiwa matengenezo, bali wanapeana taarifa kwa mdomo tu.

“Kamanda wa Takukuru leta maofisa kutoka mkoani waje wafanye ukaguzi wa kila jambo ambalo limeainishwa,” alisema.

“Hatuwezi kuacha halmashauri iendeshwe kienyeji bila kufuata taratibu. Mkalama inaonekana chafu kumbe tatizo ni mtu mmoja, mnasaini vocha halafu mnamsingizia RAS?

“Ajenda ya kikao changu nanyi watumishi wenzangu, nilitaka tuambiane kwamba ni lazima tutunze mali na fedha za Serikali. Waheshimiwa madiwani ni lazima msimamie halmashauri yenu na mhoji kila senti imetumika vipi. Kama ni jengo nendeni mkakague, kama ni kisima nendeni mkaangalie,” alisema Waziri Mkuu.

“Pia, niwasihi waheshimiwa madiwani wenzangu, msikubali kutumika kupitisha matumizi ya fedha ambayo si sahihi. Watumishi wa halmashauri hii mfanye kazi, muache ubabaishaji kwa sababu Serikali hii iko makini sana. Msiishi kwa mazoea kwa sababu wakati siyo wenyewe na tena muache kutengeneza syndicates.”

Pia, amemuonya ofisa manunuzi wa wilaya hiyo, Dickson Mataramba aache kutumika na kufanya kazi kwa mazoea kwa kupandisha bei ya Sh2,000 hadi Sh3,000 kwenye vifaa wanavyoagiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekataa kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya kwa sababu lilikataliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge na uchunguzi wake bado haujakamilika.

“Jiwe la msingi mlilonipangia kuweka leo (jana) kwenye hospitali ya wilaya siweki hadi Takukuru wakamilishe kazi ya uchunguzi kuhusu mikataba iliyotumika. Mkikamilisha uchunguzi mniite, nitakuja kulizindua likiwa limekamilika,” alisema.

Source: mwananchi