Mnyeti awaonya wanasiasa Simanjiro

0
32
By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewashukia baadhi ya wanasiasa wilayani Simanjiro wanaowagawa wananchi katika makundi kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa ili wapate nafasi kuwania ubunge mwaka 2020 kwa tiketi ya CCM.

Mnyeti ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 kwenye kijiji cha Narakauo katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano wilayani Simanjiro.

Amesema wanasiasa uchwara wilayani humo wanaotumia makundi wanayoyaunda kugawa wananchi ili wafanikiwe kuwania ubunge wamefikia mwisho.

“Mimi ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa ndio sababu Oktoba 3 tukafuta mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ndani ya CCM wilayani Simanjiro na kuagiza uanze upya kwa lengo la kuondokana na ubabaishaji,” amesema Mnyeti.

Amesema walibaini baadhi ya wenye uchu wa kugombea ubunge walitaka kucheza mchezo mchafu kwa kukata majina na kupitisha watu wao.

Advertisement

“Hii itakuwa maalum kwa Simanjiro wagombea wote  watapitishwa hakuna kukata jina la mtu wote wakapigiwe kura na kuamuliwa huko,” amesema.

Amesema wananchi wa wilaya ya Simanjiro hivi sasa wanataka maendeleo hawahitaji siasa uchwara zisizo na mwelekeo wenye manufaa kwao kwa kutumia nafasi ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula amewataka wananchi wa eneo hilo kutowachagua viongozi wanaojihusisha na uuzaji wa ardhi ili kuepusha migogoro ya ardhi.

Mkazi wa kijiji cha Narakauo,  Mosses Ole Sanjiro amemshukuru Mnyeti kwa kuagiza kijiji hicho kipatiwe mawasiliano ya simu kwani awali walikuwa hawana mawasiliano.

Source: mwananchi