Vituko vinavyofanywa na viongozi wateule

0
37
By Mwandishi Wetu,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akitimiza miaka minne madarakani, baadhi ya wateule wake katika nafasi mbalimbali wamekuwa wakifanya matukio yanayoibua hisia hasi kwa umma.

Matukio hayo yanafanywa na baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na kuibua gumzo mitaani na hasa kwenye mitandao ya kijamii ambako kumekuwa kimbilio la mijadala kuhusu masuala mbalimbali.

Mwendelezo wa matukio hayo, ambayo baadhi huonekana kama vituko, ulifanywa na mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila aliyekwenda shuleni kuwacharaza viboko wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiwanja wanaotuhumiwa kuhusika katika mabweni mawili kuungua.

Chalamila aliwachapa wanafunzi 14 wa kidato cha tano na sita viboko vitatu kila mmoja kwa tuhuma za kuhusika kuchoma mabweni.

Mkuu huyo wa mkoa alihusisha tukio la wanafunzi hao kukutwa na simu na moto huo, akisema walichukia baada ya kunyang’anywa simu zao.

Tukio hilo ndilo lililoibua mjadala mkubwa wiki hii, wengi wakimkosoa mkuu huyo kwa kuadhibu kabla ya tuhuma kuthibitika na wengine wakikosoa kitendo chake cha kuamua kuwachapa wakati sheria inakataza mtu asiye mwalimu mkuu au aliyeteuliwa na mwalimu kutekeleza adhabu hiyo.

Advertisement

Hata hivyo, Rais Magufuli amemkingia kifua Chalamila, kutokana na watoto hao kuhusishwa na uchomaji wa bweni na akasema anatamani mkuu huyo angewachapa viboko zaidi.

Hilo ni moja ya matukio ya Chalamila. Siku chache zilizopita, alitoa kauli iliyoibua utata wa kisheria baada ya kuwaambia wananchi mwizi anayevunja nyumba kuingia ndani, hakuna njia nyingine bali ni kumuua kwanza kwa kuwa ni hatari.

Watetezi wa utawala wa sheria walimkosoa kuwa kauli hiyo inachochea watu kujichukulia hatua mkononi na kwamba ingeweza kusababisha watu wafanyiane ubaya na kutumia kisingizio kuwa mmoja alivamia nyumba ya mwingine.

Mbali na tukio hilo, Chalamila aliibua mjadala mwingine alipomweleza Rais miezi minne iliyopita kuwa mshahara anaompa unamtosha hata kumuwezesha kukaa na hawara, maarufu kama mchepuko.

Chalamila ni mmoja wa viongozi wanaotoa kauli tata zinazolalamikiwa na makundi tofauti katika jamii.

Agosti 26, 2019, mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri alikaririwa na vyombo vya habari akitaka watuhumiwa wa wizi wavunjwe miguu. Alitoa kauli hiyo alipokuwa katika kikao cha madiwani hivi karibuni.

“Tumekuwa tukikamata wadokozi wengi na vibaka wengi. Tunapowapeleka mahakamani kesi hizo zinakuwa hadithi, wanapewa dhamana wanatolewa,” alisema akionyesha wasiwasi wa mamlaka zinazosimamia utoaji haki.

“Kwa hiyo imekuwa ni hadithi wakirudi wanaendelea na shughuli zao. Safari hii ninawatangazia, tutavunja miguu, tutawakamata tutawapiga, tutawavunja miguu na tutawaweka ulemavu.

“Sheria inakataa tusiwapige na sheria inakataa wasiibe. Sasa muda ukifika tutajadili, kipi kianze. Ndiyo maana nasema kwamba nawashurkuru wananchi wangu wa wilaya ya Kigamboni wamenielewa vizuri sana na mpaka sasa tutapata ushirikiano wa kutosha.”

Kauli hiyo pia imekosolewa na watetezi wa haki za binadamu na utawala wa sheria ambao wanasema chombo pekee kinachomtia hatiani mtuhumiwa ni mahakama.

Jeshi la Polisi limekuwa likishauri wananchi kutojichukulia sheria mkononi kunapotokea wahalifu na kutaka wafikishwe polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria.

DC Kilolo na madereva 10

Mteule mwingine ambaye ameingia katika vinywa vya watu ni mkuu wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdalah ambaye amebadilisha hadi madereva 10 ndani ya miaka minne.

Jambo hilo lilimshtua Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake mkoani Iringa na kumuagiza mkuu wa mkoa, Ally Happi kuchunguza utendaji kazi wa mteule huyo.

Hata hivyo, madereva wawili wa zamani wa mkuu huyo wa wilaya, walimtuhumu bosi huyo kukosa staha katika matamshi na kutoa lugha chafu kwa madereva.

Madereva hao walidai bosi wao huyo huingia kwenye gari bila kuwapa utaratibu wowote, bila kusema anakokwenda na hata anapofikishwa nyumbani, hushuka kimyakimya bila kusema asante wala kwaheri.

Amri ya DC Bariadi ilivyogeka kituko

Pia mwezi uliopita, mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Festo Kiswaga naye aliingia katika orodha ya viongozi waliotoa amri iliyoonekana kuwa kituko na baadaye ikatenguliwa.

Mkuu huyo aliagiza watumishi wote 137 wa hospitali ya Halmashauri ya mji wa Bariadi ya Somanda, wakatwe mishahara yao ili mashine iliyoibwa ya Ultrasound inunuliwe.

Amri hiyo iliibua hisia hasi kutokana na kutofanyika uchunguzi kubaini mwizi na badala yake wafanyakazi wote kubebeshwa mzigo.

Ndani ya saa 24 tangu kutolewa kwa amri hiyo, katibu tawala wa Simiyu (RAS), Jumanne Sagini alijitokeza na kusema haiwezekani watumishi wote wakaiba kifaa hicho na kutengua agizo hilo.

RAS huyo alisema amri ya DC ikitekelezwa itakuwa inaingilia majukumu ya vyombo vya uchunguzi na kutaka suala hilo lifanyiwe kazi na vyombo vya dola.

Source: mwananchi