Auawa na polisi akidaiwa kutaka kuiba vifaa vya ujenzi

0
21
By Jesse Mikofu, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Mtu mmoja anayedaiwa kuwa jambazi ameuawa na polisi mkoani Mwanza akidaiwa kuwa alikuwa akifanya jaribio la kuiba vifaa vya ujenzi katika ghala mali ya Charles Faida wilayani Nyamagana mkoani Mwanza
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 8, 2019 na Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza,  Jumanne Muliro inaeleza kwamba tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo katika mtaa wa Tanesco Igogo.
Muliro watu watano wanaodaiwa kuwa majambazi waliwavamia walinzi wa ghala hilo na kuwafunga kamba miguuni, kuvunja na kuanza kuiba vifaa hivyo.
“Wakati wakiendelea kutoa vifaa nje askari waliokuwa doria walipata taarifa na  walifanya haraka kufika eneo hilo.”
“Walipofika jambazi aliyekuwa ameshikilia silaha aina ya Shotgun akawafyatulia risasi askari lakini wakamkabili kwa kumpiga risasi na amefariki dunia akipelekwa hospitali,” amesema Muliro
Katika tukio hilo pia walikamata silaha Shotgun iliyofutwa namba ikiwa na risasi tatu, mkasi, nondo na mapanga mawili.
Amesema mwili umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando, kwamba msako unaendelea kuwakamata wengine.

Source: mwananchi