Majaliwa kuupokea mwenge Ruangwa

0
44
By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amewasili wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi kwa ajili ya kushiriki mbio za mwenge kitaifa.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 9, 2019 na ofisi ya waziri mkuu inaeleza kuwa mwenge huo tayari umewasili mkoani humo na Majaliwa ataungana na wananchi kushiriki katika mbio hizo.

Akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali mara baada ya kuwasili mkoani humo Majaliwa amesema, “Kesho nitaungana na wananchi wa wilayani Ruangwa ili kesho kutwa (mwenge) uendelee wilaya ya Nachingwea.”

Majaliwa ambaye pia mbunge wa Ruangwa amesema amefurahishwa na hamasa waliyonayo wananchi katika mapokezi ya mwenge huo huku akibainisha kuwa miongoni mwa wageni katika mbio hizo ni Rais John Magufuli.

Amesema mbali na maadhimisho ya kumaliza mbio za mwenge nchi nzima, Tanzania pia inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere.

“Tuendelee kuwahamasisha wananchi wa Lindi na Watanzania wote washiriki kwenye makongamano yanayofanyika nchini kote. Kumbukumbu ya Baba wa Taifa isaidie kuelimisha vijana wetu  ambao hawajui historia ya kazi za waasisi wa Taifa letu.”

Advertisement

“Pia walioko madarakani,  watumie fursa hii. Waige na kuenzi kazi za viongozi kama Mwalimu Nyerere na pia wajenge tabia ya kujua tabia ya walipotoka, na mahali walipo.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,  Jenista Mhagama amesema mbio hizo zilianza Aprili 2, 2019.

Amesema hadi Oktoba  14, 2019 siku ya kilele utakuwa umepita katika Halmashauri 195 nchi mzima,”katika kipindi hicho chote, vijana wetu sita ambao ni wakimbiza mwenge walizindua miradi ambayo wameridhika nayo na ile yenye dosari hawakusita kuikemea.”

Amesema makongamano mbalimbali yameandaliwa ili kuenzi kifo cha Baba wa Taifa ambaye Oktoba 14, atatimiza miaka 20. Pia vijana 88 ambao walipanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu hizo watashiriki sherehe hizo.

Source: mwananchi