Mbowe kuongoza waombolezaji Mwanakotide akiagwa Dar es Salaam

0
43
By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kesho Jumatano Oktoba 9, 2019 ataongoza waombolezaji kuaga mwili wa kada wa chama hicho, Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotode.

Shughuli za kuaga mwili wa Mwanakotide zitafanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Moyo wa Mtakatifu wa Yesu, Manzese jijini Dar es Salaam.

Mwanakotide alifariki dunia Jumapili Oktoba 6, 2019 katika Hospitali ya St Monica, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.

Alikuwa mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za hamasa za chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kujizolea umaarufu kupitia mikutano ya hadhara ya chama hicho, zikiwemo kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na 2015.

Akizungumza leo mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene amesema utoaji wa heshima za mwisho utakwenda sambamba na kutoa salamu za rambirambi kutoka makundi mbalimbali.

“Shughuli za kuuga mwili zitakayofanyika kanisani hapo kuanzia saa 6 mchana, baada ya mwili kuchukuliwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala ulikohifadhiwa.”

Advertisement

“Safari ya kuusindikiza mwili wa Mwanakotide kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Ruvuma itaanza Jumatano  mazishi yatafanyika Ijumaa Oktoba 10, 2019, katika kijiji cha Lituhi, Nyasa,” amesema Makene.

Mbowe alikuwa miongoni mwa wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania walioshiriki msiba wa msanii huyo Mikocheni A jijini Dar es Salaam.

Source: mwananchi