Mshtakiwa kesi ya Maimu wa Nida akiri makosa

0
24
By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Astery Ndege, mshtakiwa wa tatu katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili  na wenzake watano akiwemo aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kurejesha  serikalini Sh293.4 milioni.

Ndege ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers anarejesha kiasi hicho cha fedha ikiwa ni sehemu ya hasara iliyosababishwa na washtakiwa hao ya Sh1.175 bilioni.

Akitoa hukumu hiyo leo Jumanne Oktoba 8, 2019  Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally amesema mshtakiwa huyo atalipa fedha hizo kwa mujibu wa makubaliano kama sehemu ya fidia ya hasara aliyoisababisha.

Mbali na adhabu hiyo, Hakimu Ally ameamuru mshtakiwa Ndege kulipa  faini ya Sh4 milioni  na akishindwa atatumikia kifungo cha miaka 20  jela.

Amesema ametoa hukumu hiyo baada ya kuzingatia kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza, amekiri akiashiria kujutia kosa lake.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Ladslaus Komanya amesema hawana kumbukumbu za makosa ya  nyuma ya mshtakiwa huyo, kwamba ni mkosaji kwa mara ya kwanza.

Advertisement

Komanya aliieleza mahakama wakati ikifikiria kutoa adhabu atazame utaratibu alioutumia kukiri kosa kwa mshtakiwa  kwa kuwa umepunguza taratibu nyingi za jinai.

Pia imesaidia katika kampeni ya kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani.

Wakili wa mshtakiwa huyo, Godwin Nyaisa aliungana na upande wa mashtaka kuwa mshtakiwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza na amekaa mahabusu kwa miezi 10, “ameonja ladha ya gereza, mahakama itoe adhabu ya faini.”

Ndege ambaye ni mshtakiwa wa tatu kati ya washtakiwa sita ataanza kulipa Sh50 milioni kwa awamu ya kwanza.

Awali, kabla ya kusomwa kwa barua yake ya kukiri makosa,  wakili Komanya aliwasomea mashtaka mapya washtakiwa hao ambayo yalipungua kutoka 100 ya awali hadi 50.

Wakati wa usomwaji wa mashtaka hayo Maimu na wenzake watano waliyakana mashtaka yote lakini Ndege alikiri na kusomewa maelezo ya awali, kisha akatiwa hatiani na kuhukumiwa.

Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili Maimu na wenzake wanne ni kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni.

Mengine ni utakatishaji fedha, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri wao  na kuisababishia mamlaka hiyo hasara, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Mbali na Maimu washtakiwa wengine  ni meneja biashara wa Nida, Aveln Momburi; ofisa usafirishaji, George Ntalima; mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na Oktoba 15, 2019 itatolewa tarehe ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Source: mwananchi