Serikali ya Tanzania kuwalipa wakulima wa korosho Sh59 bilioni kabla ya Novemba 2019

0
27
By Haika Kimaro, Mwananchi [email protected]

Mtwara. Naibu Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Omary Mgumba amesema wakulima wa korosho ambao hawajalipwa Sh 59 bilioni za mauzo ya zao hilo  msimu wa  2018/19 hadi kufikia Oktoba 31, 2019 watakuwa wamelipwa.

Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa korosho mkoani Mtwara, amesema katika msimu huo walikusanya korosho tani 222,000  zilizokuwa na thamani zaidi ya Sh722 bilioni na kwa sasa baadhi ya wakulima wanaidai serikali Sh 59 bilioni.

 “Mpaka sasa tumeshalipa zaidi ya 663 bilioni bado kuna wakulima wanadai zaidi ya Sh59 bilioni na tunafahamu kuna zaidi ya Sh24 bilioni za watoa huduma wanadai. Niwahakikishie wadau wote wanaoidai Serikali mpaka kufikia Oktoba 30, 2019 watakuwa wamelipwa,” amesema Mgumba

Mgumba amesema katika msimu wa 2017/18 zao hilo liliingizia Taifa Sh1.3 trilioni  ikiwa ni fedha nyingi kuliko zilizopatikana katika mazao ya kahawa, pamba na madini.

Aidha ametolea ufafanuzi wa taarifa zinazosambazwa kwamba Serikali itanunua tena korosho msimu wa mwaka 2019/20 na kusema haina nia  hiyo  na endapo bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko itanunua zao hilo itanunua kama wanunuzi wengine wote.

Amesema katika msimu wa mwaka 2019/20 wanatarajia kuzalisha zaidi ya tani 290,000 na kwamba maandalizi yote yamekamilika kasoro mkutano wa wadau.

Advertisement

Amesema mikakati iliyopo ni kuzalisha tani 1 milioni  ifikapo 2023/24  na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa uzalishaji duniani.

Kaimu Mkurugenzi wa bodi ya korosho (CBT), Francis Alfred amesema bado matumizi ya pembejeo kwa wakulima yapo chini licha ya makadirio ya msimu kuwa juu.

Amesema katika msimu wa mwaka 2019/20 mahitaji yalikadiriwa kuwa tani 30,000 za salfa ya unga na lita 350,000 za viuatilifu maji.

“Mpaka Septemba 2019 salfa iliyotumika ni tani 2,610 na viuatili tani 159,000. Hii inaonyesha makadirio yako juu na matumizi ya pembejeo yako chini, kiasi kilichotumika ni chini ya asilimia 50 ya makadirio bado kuna fursa ya kuongeza tija ya wakulima iwapo kutakuwa na matumizi sahihi ya viuatilifu,” amesema Alfred.

Source: mwananchi