Hatua ya kwanza ujenzi hospitali wilaya ya Kigamboni yakamilika

0
19
By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni imekamilisha hatua ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo kwa gharama ya Sh1.5 bilioni.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ng’ulwabuzu Ludigija amesema hayo leo Jumanne Oktoba  8, 2019 katika ziara ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwamba ujenzi wa majengo saba kwenye hospitali hiyo umeshakamilika.

Ametaja majengo hayo kuwa ni utawala, maabara, stoo ya dawa, jengo la Xray na la kufulia nguo.

“Siwezi kuahidi ni lini hospitali hii itaanza kufanya kazi lakini kwa sasa tunakamilisha vitu vyote vya muhimu,” amesema Ludigija.

Awali,  Makonda amesema pamoja na kukamilisha hatua ya kwanza ya ujenzi, wanatakiwa kuandaa mazingira ‘land scarping’ kwa kupanda miti, majani na kutengeneza njia nzuri za kupita wagonjwa zinazounganisha majengo hayo.

Amesema mkakati uliopo kwa sasa ni ujenzi wa stendi ya mabasi ili iwe rahisi kwa wananchi kuzifikia huduma mbalimbali ikiwamo ya afya bila usumbufu.

Advertisement

Kwa sasa wananchi wa Kigamboni wanategemea kupatiwa huduma kituo cha afya cha vijibweni ambacho kilipandishwa hadhi na kutumika kama hospitali ya wilaya kwa kuwahudumia wakazi wa eneo hilo na maeneo ya jirani.

Source: mwananchi